come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

KIPUTE LIGI KUU KUANZA AGOSTI 24

Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara msimu ujao wa mwaka 2014/2015 inatarajia kuanza kutimua vumbi Agosti 24 kwenye viwanja mbalimbali nchini.

Hata hivyo kabla ya mechi hiyo, kanuni za ligi zinasema kwamba inatakiwa itanguliwe na mchezo wa kuwania Ngao ya Hisani ambao humkutanisha bingwa mtetezi na mshindi wa pili wa msimu uliopita (Azam vs Yanga).


Azam ndiyo bingwa mtetezi wa ligi hiyo inayotoa wawakilishi wa Tanzania Bara katika mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Afisa Habari na Mawasiliano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema kuwa klabu zote 14 zinazotarajiwa kushiriki ligi hiyo zinatakiwa kuanza maandalizi mapema ili kuifanya ligi iwe na ushindani.

Wambura alisema kwamba ratiba ya ligi hiyo bado inafanyiwa kazi na itakapokuwa imekamilika itatangazwa.

Timu 14 zitakazoshiriki ligi hiyo ni pamoja na Azam, Yanga, Simba, Mbeya City, Kagera Sugar, Mtibwa Sugar, JKT Ruvu, Ruvu Shooting, Coastal Union, JKT Mgambo na Prisons.

Klabu nyingine ambazo zimepanda daraja msimu huu ni Ndanda FC ya Mtwara, Polisi Morogoro na Stand United ya mkoani Shinyanga.

Ligi hiyo pia hutoa mwakilishi wa Bara katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) yanayoandaliwa kila mwaka na Shirikisho la Soka la ukanda huo (CECAFA).

Azam iliyoanza kushiriki ligi ya Bara msimu wa mwaka 2008/2009 ilitangazwa bingwa kwa mara ya kwanza Aprili 13 na kumaliza 'ubabe' wa klabu za Simba na Yanga zilizokuwa zimetawala na kupokezana kutwaa ubingwa huo kwa miaka 10.