IKIWA tayari imemsajili winga Mrisho Ngasa, kocha wa Yanga, Ernest Brandts
amesema timu yake inahitaji wachezaji watatu tu zaidi ili kuimarisha
kikosi chake cha msimu ujao.
Akizungumza na gmtandao huu jana, Brandts
alisema mipango yake ilikuwa kusajili wachezaji wanne wapya kwenye timu
hiyo katika kipindi hiki cha usajili na baada ya kumnasa Ngasa, mkakati
ni kuongeza wachezaji wengine watatu.
Alisema kuwa wachezaji anaowataka katika timu hiyo ni mshambuliaji mmoja, mlinzi mmoja na golikipa mmoja mwenye uzoefu.
"Moja ya mipango yangu nimekamilika kwa kumsajili Ngasa," alisema kocha huyo raia wa Uholanzi.
"Lakini nilishatoa mapendekezo yangu na
mikakati yangu kwa viongozi miezi miwili iliyopita ya kutaka kuongeza
wachezaji watatu zaidi na tunaendelea kufanyia kazi jambo hilo kwa
kushirikiana na uongozi wa klabu."
Alisema golikipa namba moja wa sasa wa
kikosi chake Ally Mustapha 'Bartez' anahitaji msaidizi mwenye uzoefu
ambaye atakauwa akipokezazna naye kukaa langoni.
Huku akificha majina, Brandts alisema wapo
wachezaji aliowaona kwenye ligi kuu kutoka timu nyingine ambao
angependa kuona wanasajiliwa kikosini hapo katika kukiimarisha kikosi
chake.
"Suala la wachezaji gani wasajiliwse
nafikiri ni jambo langu na uongozi lakini wapo wachezaji hapa (Tanzania)
ambao nimeona wana uwezo wa kuichezea Yanga."
Hata hivyo, pamoja na mwalimu huyo
kutotaja majina, Yanga imekuwa ikihusishwa na kumchukua kiungo wa Simba
na Taifa Stars Amri Kiemba kuwa miongoni mwa wachezaji hao watatu.
Yanga ipo katika mkakati wa kukiimarisha
zaidi kikosi cha timu hiyo kilichotwaa ubingwa wa ligi kuu ya Bara msimu
uliomalizika Mei 18.