come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

FEDHA ZA OKWI, SIMBA YAPIGWA DANADANA

KLABU ya Simba bado imeendelea kusotea fedha za mshambuliaji wake, Emmanuel Okwi anayechezea klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia na Juni 15 watajua hatima ya fedha hizo.
Okwi aliuzwa Etoile mapema mwaka huu kwa kitita cha Dola za Marekani 300,000 (Sh500 milioni) na kulipwa mshahara wa dola 15,000 (Sh24 milioni) mwa mwezi.
Akizungumza na mtandao huu mwishoni mwa wiki, Makamu Mwenyekiti wa Simba, Joseph Itang’ale alisema tayari wameandika barua TFF na Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) kuomba msaada ili walipwe fedha hizo.
“Tulishaandika barua toka mwezi uliopita, tumeambiwa tuvute subira mpaka Juni 15, huenda fedha hizo zitakuwa zimeshaingia,” alisema.
Itang’ale alisema mpaka kufikia tarehe hiyo kama hawatalipwa pesa zao, watajua nini cha kufanya.
“Ni muda mrefu sasa toka watuahidi kutulipa na hakuna walilotekeleza mpaka sasa,” alisema na kuongeza. “Tumekuwa tukiwafuatilia kila wakati kwa lengo la kuwakumbusha kuhusu pesa hizo.”
Alisema majibu waliyokuwa wakipewa hayawaridhishi ndiyo maana wameamua kuandika barua ngazi za juu kuomba msaada.
“Wanajitetea kwa kusema nchini kwao kuna vuguvugu za kisiasa jambo ambalo ni vigumu kuhamisha pesa,” alisema Itang’ale.