MASHUJAA Band iliuteka usiku wa Tuzo za Kilimanjaro Muziki kwa
kunyakua tuzo tano kwenye Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam
juzi usiku. Mashujaa wanaotamba na wimbo wao wa Risasi Kidole walinyakua
Tuzo ya Msanii Bora wa Kiume wa Bendi iliyokwenda kwa Charz Baba pamoja
na ile ya Mtunzi Bora wa Mashairi ya Bendi wakati ya Rapa Bora
ilikwenda kwa Fergason.
Tuzo ya nne iliyoibeba bendi hiyo yenye maskani
yake Vingunguti na kuwabwaga wapinzani wao ni ile ya Wimbo Bora wa Bendi
kupitia wimbo wao wa Risasi Kidole ambao walichuana na Mapacha Watatu
(Chanzo ni Sisi), Shamba la Twanga (African Stars) na Jinamizi la Talaka
(Mlimani Park).
Mashujaa walifunga kazi baada ya kutwaa Tuzo ya
Bendi Bora ya mwaka ambayo walikuwa wakiwania na Twanga Pepeta, Mapacha
Watatu, Msondo Ngoma na Mlimani Orchestra ‘Sikinde’. Wasanii wengine
waliong’ara kwenye tuzo hizo ni Kalla Jeremia sambamba na Ommy Dimpoz
ambao wote kila mmoja aliondoka na tuzo tatu.
Kalla Jeremiah alinyakua tuzo ya wimbo bora wa
mwaka (Dear God), Mtunzi Bora wa Mashairi wa Hip Pop na Msanii Bora wa
Hip Pop, wakati Dimpoz alinyakua ya Tuzo Video Bora ya Wimbo wa Mwaka
(Baadaye), Wimbo Bora wa Bongo Pop na Wimbo Bora wa Kushirikiana wa Me
and U ambao alimshirikisha Vanesa Mdee, huku tuzo kubwa kabisa ya All
Fame (Waliochangia mafanikio ya muziki) ikienda kwa Kilimanjaro Band
‘Wana Njenje.’