Katibu Mkuu wa Cecafa, Nicholaus Musonye ameenda
mbali zaidi kwa kusisitiza kwamba hawana mpango wa kubadilisha vituo vya
Darfur kwavile mechi zote zitachezwa huko na hakuna mechi itakayochezwa
mjini Khartoum.
Simba na Yanga ni miongoni mwa timu 13
zinazoshiriki Kombe la Kagame ambayo itachezwa kwenye miji ya Al Fashir
na Kaduqli iliyoko Darfur Kaskazini ambako awali kulikuwa ngome za waasi
na kumekuwa kukiripotiwa matukio kadhaa ya uvunjifu wa amani na usalama
wa raia.
Musonye aliuambia mtandao huu jana Jumatatu kwamba;
"Haya mambo mengine muache siasa, hiyo miji yote ina amani kabisa na
nilishawaandikia Simba na Yanga pamoja na timu zote zinazishiriki kwamba
usalama upo wa kutosha kabisa."
"Mimi nimelala kule siku tatu na wala sikupata
usumbufu wowote, kuna amani kabisa. Na hoteli tulizowaweka Simba na
Yanga ni za hali ya juu sana acheni siasa, timu zote zitakuwa kwenye
hiyo miji wala hakuna mabadiliko yoyote tutakayofanya, acheni
siasa,"alisisitiza Musonye akikanusha tamko la Waziri wa Mambo ya Nje wa
Tanzania, Bernard Membe alilotoa Bungeni Jumamosi kwamba Darfur si
sehemu salama.