YANGA imewasainisha mastraika wawili. Mmoja wao ni Shabaan Kondo
aliyefanya mazoezi siku tatu na Simba wiki iliyopita na imedai kwamba
kwa kiwango alichonacho atachukua namba ya Mbwana Samatta ndani ya Taifa
Stars.
Straika mwingine ametokea klabu ya Machava ya
Moshi, Kilimanjaro inayoshiriki Daraja la Kwanza ambaye umri wake na
kiwango chake ndiyo kigezo kilichombeba.
Kigogo mwenye ushawishi mkubwa kwenye usajili wa
Yanga, aliuambia mtandao huu jana Jumatatu kwamba; "Tumesaini mastraika
wawili, mmoja Kondo na mwingine anachezea Machava, ni vijana wadogo
chini ya miaka 21, huyo Kondo tulimchomoa Simba alifanya nao mazoezi
tangu Jumanne mpaka Alhamisi."
"Ni mchezaji mwenye mwili mzuri na uwezo mkubwa
sana, tumemuona kwenye ligi ya Msumbiji na ninakuhakikishia ndiye
straika ambaye anakuja kuchukua namba ya Samatta Taifa Stars, ngoja
aanze kucheza utakubali maneno yangu. Yanga hatubahatishi safari hii,
"alisisitiza kiongozi huyo.
Kondo alifanya mazoezi na Simba katika Uwanja wa
Kinesi, Dar es Salaam kwa siku tatu wiki iliyopita, lakini 'akaibiwa' na
viongozi wa Yanga.
Alisema kwamba picha nzima ya usajili wa Yanga
itajulikana kabla ya wikiendi hii kwani Kocha Mkuu Ernest Brandts
atakuwa amewasili kuendelea na progamu ya kuiandaa timu ambayo ilianza
mazoezi mepesi jana Jumatatu chini ya Kocha Msaidizi Fred Minziro.
Kiongozi huyo alisema kwamba hawawezi kusajili
wachezaji zaidi ya watano kwenye usajili huu kwavile timu yao ni imara
na inahitaji mabadiliko madogo ya kujiimarisha tayari kwa Kombe la
Kagame na Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani.
Wakati Yanga ikisajili wawili tayari Simba
imeshasaini wachezaji zaidi ya 10 wa ndani baadhi yao wakiwa wale wa
zamani walioongozewa mikataba na chipuzi ni wengi zaidi.