Ngwair alifariki wiki iliyopita nchini Afrika
Kusini alikokwenda kwa shughuli za muziki na mwili wake kuletwa jana
mchana, Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere Dar es Salaam.
Simanzi ilitanda eneo zima la uwanja walikojazama
mashabiki wa sanaa ya muziki, wengi wao wakiwa vijana wakati jeneza la
Ngweair likitolewa sehemu ya ndani ya uwanja na kuletwa nje.
Vilio pia vilitawala kutoka kwa ndugu wa marehemu
na watu wengine walioshindwa kuvumilia baada ya kushuhudia jeneza hilo
likitolewa nje tayari kwa safari ya kupelekwa Hospitali ya Taifa,
Muhimbili.
Kutokana na wingi wa watu, vijana wa skauti
walilazimika kufanya kazi ya ziada kuunganisha mikono yao ili gari
lililobeba mwili wa Mangwair liweze kupita bila kuzongwa, jambo
lililowashinda nguvu.
Hali ilikuwa tofauti baada ya kundi la vijana
kuendelea kuimba wimbo wa Kamanda, huku wakisukuma gari lililobeba mwili
wa Ngwair na kusababisha msongamano mkubwa wa magari.
Kadri mwili wa msanii huyo ulivyokuwa ukisogea
mbele, ndivyo watu hasa vijana walivyokuwa wakijitokeza kutoka pembezoni
mwa barabara na kuungana na wengine kusukuma gari.
Kazi ya kusukuma gari hiyo iliendelea kwa muda
mrefu kupita barabara kuu ya Pugu kuelekea Muhimbili, ambako mwili wake
ungehifadhiwa kabla ya kuagwa.
Rais wa Shirikisho la Muziki Tanzania, Ado Novemba
alisema mwili wa marehemu utaagwa leo kwenye Viwanja vya Leaders Club,
Kinondoni kuanzia saa mbili asubuhi mpaka saa sita mchana.
Baada ya hapo, marehemu atasafirishwa kwenda Morogoro kwa ajili ya mazishi yatakayofanyika kwenye makaburi ya Kihonda.
Awali, mwili wa Ngwair mwimbaji wa kibao ‘Mikasi’,
ulitarajia kuwasili mwishoni mwa wiki iliyopita, lakini ilishindikana
kutoka na sababu za kitaalamu kulazimisha mwili huo kupimwa ili kujua
chanzo cha kifo chake