MASIKINI!, Azam FC imewatoa kwa mkopo wa kwa heri kwa kiungo wake mkongwe Abdi Kassim ‘Babi’ na kumtema mshambuliaji wake Uhuru Seleiman aliyekuwa kwa mkopo akitokea Simba SC.
Meneja wa timu hiyo, Patrick Kahemela alisema
jana kuwa sababu kubwa ya kuachana na wachezaji hao ni mikataba yao
kumalizika pamoja na umri kuwatupa mikono.
Wachezaji waliotupia virago ni pamoja na Lewis
Cosmas aliyejiunga na Ruvu Shooting na Abdulhalim Humoud aliyepata timu
Afrika Kusini ya Jomo Cosmos.
Akizungumza na gazeti hili Abdi Kassim alisema
“Ni kweli mkataba wangu kuitumikia Azam umeisha ingawa walinitaka
nisaini mpya, lakini tukashindwa kuafikiana. “Naamini bado nina nguvu
na uwezo wa kucheza soka. Kwa hiyo niko tayari kujiunga na timu yoyote
ambayo itaonyesha nia ya kunitaka.” alisema Babi aliyekipiga na klabu
za Mlandege ya Zanzibar, Mtibwa Sugar, Yanga, DT Long ya Vietnam
pamoja na timu ya Taifa ‘Taifa Stars’.
Anaeleza kuwa yuko tayari kujiunga na Yanga,
Mtibwa Sugar ama Coastal Union iwapo zitaonyesha kutaka kumsajili kwa
ajili ya msimu ujao.
Klabu ya Mtibwa iliwahi kukiri kutaka kumrejesha Babi nyumbani katika dirisha dogo la usajili Januari mwaka huu.
Wachezaji wengine walioachwa na Azam ni kipa
Deogratius Munishi, Sunday Frank na Uhuru Seleiman aliyekuwa
akiitumikia klabu hiyo kwa mkopo akitokea Simba. “Munishi mkataba wake
umekwisha huku Uhuru akirejeshwa Simba, baada ya kumaliza msimu wake
wa mkopo na Azam.” alisema Kahemela.
Alieleza kuwa kama ilivyokuwa wakati wa dirisha la
uhamisho wa wachezaji msimu ulioisha Azam ilimsajili George Odhiambo
‘Blackberry’ peke yake.
“Safari hii tena tumeamua kuwapandisha wachezaji
wawili wa U-20, Mudathir Yahaya na kipa Hamadi Juma na kufunga zoezi la
usajili,”
“Kwa mujibu wa ripoti ya kocha Stewart Hall,
inaeleza hakuna sababu ya kwenda nje kusajili wachezaji ambao viwango
vyao havipishani na waliopo klabuni.” alisema kiongozi huyo.
Aidha alisema wachezaji wengine wote waliosalia
wanabaki klabuni hapo ingawa, kocha amependekeza baadhi ya vijana wa
U-20 walioonyesha viwango vya juu wapandishwe timu kubwa.