Endapo Ivory Coast yenye pointi 10
itaifunga Stars katika pambano hilo la timu mbili za kileleni mwa Kundi
C, itakuwa imefuzu kucheza hatua ya mwisho ya mtoano ya michuano ya
awali ya Kombe la Dunia kanda ya Afrika baadaye mwaka huu kwa kufikisha
pointi 13.
Lakini akizungumza na waandishi wa habari
jijini Dar es Salaam jana, kocha wa Taifa Stars yenye pointi sita huku
zikiwa zimebaki mechi mbili kwa kila timu, Mdenmark Kim Poulsen aliahidi
tena kuwa watawafunga viongozi hao wa kundi.
Akiwa amefuatana na nahodha wa timu hiyo,
Juma Kaseja, Poulsen alisema vijana wake wameiva na wapo kamili
kuwafunga mabingwa hao wa Afrika mwaka 1992. Ushindi utaiwezesha Taifa
Stars kufikisha pointi tisa.
Lakini pia Stars itakuwa katika nafasi ya
kuipiku Ivory Coast uongozi baada ya mechi za mwisho na kuingia hatua ya
mwisho ya mtoano, endapo itaifunga Gambia na wageni hao kushindwa
kuilaza Morocco katika mechi za mwisho Septemba.
"Wachezaji wako katika hali nzuri kwa
sababu kambi yetu ina umoja na kila mmoja wetu anafahamu umuhimu wa
kupata matokeo mazuri katika mechi ya kesho (leo)," alisema Poulsen.
"Tunajua mechi itakuwa ngumu kutokana na wapinzani wetu kuwa na uwezo mkubwa na wanaoongoza kwa ubora wa soka barani Afrika.
"Lakini tunaamini tutawafunga kama tulivyofanya kwa timu nyingine ngumu kama Zambia na Cameroon."
Ivory Coast hawakujitokeza katika mkutano
huo na waandishi wa habari kutokana na kile kilichoelezwa na Ofisa
Habari wa Shirikisho la Soka (TFF), Boniface Wambura, kuwa wapo kwenye
mapumziko maalum kabla ya kufanya mazoezi ya mwisho jana alasiri.
Stars itaingia uwanjani ikiwa na
kumbukumbu ya kufungwa 2-0 na Ivory Coast katika mechi ya kwanza jijini
Abidjan Juni 2 mwaka jana.
Magoli ya Tembo wa Ivory Coast,
wanaoongozwa kwa ubora wa soka Afrika huku wakikamata nafasi ya 13
duniani, yalifungwa na Salomon Kalou dakika ya 10 na Didier Drogba
dakika ya 71.
Stars itaingia uwanjani hata hivyo
ikijivunia rekodi nzuri dhidi ya timu vigogo vya soka barani kwenye
Uwanja wa Taifa katika michezo mitatu iliyopita ambapo imezifunga Zambia
1-0 Desemba 22 mwaka jana, kuipa kipigo kama hicho Cameroon Februari 6
na kuiadhibu Morocco 3-1 Machi 24.