Wakati Simba ikiendelea kusotea pesa za kuuzwa Emmanuel Okwi klabu ya Etoile du Saleh ya Tunisia, klabu hiyo imesema mpango wake wa kumpiga bei kiungo, Amri Kiemba kwenda Raja Casablanca ya Morocco utatimia iwapo klabu hiyo itakubali kutoa siyo chini ya Sh500 milioni.
Raja Casablanca imepiga hodi Msimbazi kutaka
kumsajili Kiemba baada ya kuvutiwa naye wakati walipomwona akiichezea
Timu ya Taifa (Taifa Stars) dhidi ya Morocco zaidi ya wiki moja
iliyopita.
Akizungumza na Mtandao huu jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati ya usajili ya Simba Zakaria Hanspope alisema,
kiwango hicho cha fedha ndiyo thamani ya sasa ya Kiemba.
“Tayari tumezungumza na Raja Casablanca na kweli
wameonyesha nia ya kumtaka Kiemba, lakini kwetu hakuna namna yoyote ya
kumtoa bila Sh500 milioni kuwekwa mezani,” alisema Hanspope.
“Nilipokwenda kwao (Morocco) Rais wa klabu alikuwa
Uturuki, tunasubiri arejee ili tuwatumie mchanganuo mzima wa mauzo ya
Kiemba,” alisema.
Hanspope, alisema angependa kuona klabu yake
inafanya biashara ya kuwauza wachezaji kwa faida. Tunatakiwa kuwalipa
makocha, kuingia mikataba na wachezaji, mambo yote haya yanahitaji pesa.
Hatuwezi tena kufanya biashara isiyo na faida kwa upande wetu,” alisema
zaidi bosi huyo.