Bendi ya muziki wa dansi ya African Stars 'Twanga
Pepeta' inatarajia kufanya onyesho maalum la kuwasikilizisha mashabiki
nyimbo za albamu yao ya 12 itakayozinduliwa mwishoni mwa mwezi huu.
Hayo yalisemwa na meneja wa kampuni ya Aset inayomiliki bendi hiyo
Hassan Rehan alipokuwa akizungumzia maandalizi ya uzinduzi huo na
kufafanua kuwa onyesho hilo litafanyika leo Jumatano.
"Tutafanya 'Listening Part' ili mashabiki wapate nafasi ya kusikia
nyimbo zote sita za 'Shamba la Twanga', 'Kila Nifanyalo', 'Ngumu
Kumeza', 'Mwenda Pole' na 'Nyumbani ni Nyumbani' uliobeba jina la
albamu," alisema Rehan na kuendelea:
"Wakati huu wa maandalizi ya uzinduzi wa albamu yetu tumeona
tuutumie pia kwa ajili ya kuwasikilizisha mashabiki nyimbo zote ili nao
watoe maoni yao, ndio maana tumeandaa onyesho maalum pale Billcanas."
Aliongeza kuwa bendi ya Msondo ngoma iliyokuwa imealikwa kwenye
uzinduzi wa albamu ya 'Nyumbani ni Nyumbani', haitakuwapo na badala yake
nafasi hiyo imechukuliwa na bendi ya Mlimani Park.
Meneja huyo alisema kuwa mbali na bendi ya Mlimani Park, watakuwapo
pia wasanii wa muziki wa kizazi kipya Barnaba na Linex ambao wamealikwa
kutoa burudani wakisaidiana na bendi hiyo.