Zikiwa zimebaki siku 11 ili mkataba wake na klabu ya
Simba ya jijini Dar es Salaam umalizike, kipa chaguo la kwanza ndani ya
timu hiyo na taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Juma Kaseja, amesema bado
hajasaini mkataba wa kuichezea klabu yoyote nchini na kwamba hana
wasiwasi endapo atatemwa kwenye usajili wa klabu yake ya 'Wekundu wa
Msimbazi'.
Akizungumza jana, Kaseja alisema kuwa hivi karibuni akili
yake ilikuwa katika kulitumikia taifa na atakuwa tayari kuanza
mazungumzo na klabu yoyote itakayomhitaji kuanzia Julai Mosi.
Kaseja aliyejiunga Simba mwaka 2002 akitokea Moro United ya
Morogoro na kuichezea misimu yote isipokuwa 2008/2009 alipoichezea
Yanga, alisema vilevile kuwa yeye ni mchezaji mzoefu na hakatishwi tamaa
na maneno mbalimbali yanayosemwa kuhusiana na kiwango chake.
"Bado sijafanya maamuzi yoyote, akili yangu imechoka na inahitaji
kupumzika... ila nitasema tu nitakapofanya maamuzi na kama kuwaita,
nitawaita na kuweka wazi msimamo wangu," alisema Kaseja.
Aliongeza kuwa kamwe haogopi changamoto ndani ya kikosi cha Simba
na kwamba, kusajiliwa kwa makipa wengine kwake ni faraja kwa sababu
wanaimarisha kiwango chake.
"Mimi nakuwa mzuri zaidi uwanjani kwa sababu ya ushindani wa makipa
wenzangu. Siwezi kuwa bora kama wanaonizunguka si bora, ila najua
vilevile kuwa siku hazilingani," aliongeza Kaseja.
Katika kujiandaa na msimu ujao, Simba imemsajili kipa aliyekuwa
chaguo la kwanza katika kikosi cha Kagera Sugar msimu uliopita, Andrew
Ntalla huku kipa wake wa kimataifa, Abel Dhaira, akihusishwa na mipango
ya kutaka kurejea kwao Uganda.
Kaseja ndiye nahodha na kipa chaguo la kwanza wa Taifa Stars