Siku moja baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya klabu ya
Simba Danny Manembe, kutangaza kutemwa Juma Kaseja, umeibuka mgogoro wa
chini kwa chini baada ya baadhi ya viongozi kupinga hatua hiyo.
Habari za ndani ya Simba zilizonaswa na mtandao huu zimedai kuwa uamuzi wa kamati hiyo hauungwi mkono na viongozi wote
wa Simba na baadhi ya watu wenye ushawishi mkubwa kwenye klabu hiyo.
Wanaopinga uamuzi wa kamati, wanadai kuwa Kaseja
bado ni kipa bora Tanzania kwa sasa na wanaona anastahili kuendelea
kuvaa jezi za rangi nyekundu na nyeupe.
Juzi wakati akitangaza uamuzi huo, Mwenyekiti
Manembe alisema kuwa klabu yao ina makipa watatu wapya, hivyo hawana
tena sababu ya kuendelea na Kaseja.
Makipa waliopo Simba kwa sasa ni Abel Thaira,
Andrew Ntala aliyesajiliwa kutoka Kagera Sugar na Abuu Magube
aliyepandishwa kutoka kikosi B.
“Tuna makipa watatu, hawa ni wengi sana kwetu.
Hatuwezi tena kuongeza kipa mwingine, hivyo Kaseja tunaachana naye,”
alisema Manembe.
Akiongeza, Manembe alisema kocha mpya Simba
Abdallah Kibadeni katika orodha ya wachezaji anaowataka kwa ajili ya
msimu ujao, hakumjumuisha Kaseja hivyo na wao wameamua kuachana naye.
Mmoja wa viongozi wa Simba ambaye hakutaka jina
lake kuandikwa kwenye gazeti alisema: “Kamati yote ya utendaji haimtaki
Kaseja ila Mwenyekiti wa Kamati ya usajili Hanspope (Zakari) na baadhi
ya Friends wa Simba wanamuhitaji.”
Aliongeza:”Kwa namna hali ilivyo, Hanspope peke
yake hawezi kutengua uamuzi wa kamati ya utendaji, sasa kilichobaki ni
maneno ya chinichini.”
Mtoa habari huyo alisema, yeye binafsi hana shida
na Kaseja na anamkubali kuwa ni kipa bora kwa sasa Tanzania na ndiyo
maana amepewa unahodha.
“Mimi nipo ndani ya Simba lakini ukiniuliza kwa
nini wenzangu wanamchukia Juma siwezi kujua binafsi nilishahoji hakuna
sababu yoyote ya maana sana sana ni chuki tu,” alisema.
Mbali na suala hilo la Kaseja, pia viongozi
wanadaiwa wakirushiana maneno kuhusu suala zima la usajili, ambalo
limekuwa likiendeshwa kwa mali kauli kwa baadhi ya wachezaji hususan
wanaopandishwa kutoka kikosi cha Simba B.