Wachezaji wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa
Stars, wakiwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere jijini Dar es
Salaam jana alfajiri wakitokea Morocco walikofungwa 2-1 katika mechi ya
awali ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2014. Kocha wa Stars, Kim
Poulsen alisema jana timu hiyo inaanza mazoezi leo kwa ajili ya
kuikabili Ivory Coast Dar es Salaam Jumapili hii.
Akizungumza na mtandao huu jana jijini Dar es Salaam, kocha wa Stars,
Mdenmark Kim Poulsen alisema kuwa baada ya kurejea jijini Dar es Salaam,
vijana wake walipata mapumziko ya siku moja na leo wataripoti na kuanza
kujifua kwa nia ya kuhakikisha kuwa wanafanya vizuri dhidi ya Ivory
Coast wanaoongoza katika kundi lao la C.
Alisema kuwa kikosi chake kitakuwa kinafanya mazoezi mara mbili, asubuhi na jioni kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
“Wachezaji wanafahamu kuwa Ivory Coast ni timu nzuri na ndiyo
wanaoongoza kwa ubora wa soka Afrika. Na wanatambua umuhimu wa kushinda
mechi ijayo hivyo kila mmoja amepania kujiweka vizuri kwa kabla ya mechi
hiyo,” alisema Poulsen ambaye kikosi chake kililala ugenini kwa mabao
2-1 licha ya kuonyesha kiwango cha juu dhidi ya dhidi ya mabingwa wa
Afrika wa mwaka 1976, Morocco.