MSHAMBULIAJI
wa zamani wa Simba SC ya Dar es Salaam, Abdallah Msamba amefariki dunia
usiku wa kuamkia leo nyumbani kwake Mbezi, Dar es Salaam.
Kwa
mujibu wa mchezaji mwenzake wa zamani wa Simba SC, Madaraka Suleiman
‘Mzee wa Kimyinio’, Msamba alifariki usiku manane na taarifa wamezipata
kutoka kwa mke wake.
“Babu
Msamba hatupo naye, nimetoka kupigiwa simu na Kipese (Thomas) sasa
hivi, kwamba kapigiwa simu na mkewe juu ya msiba wa Msamba,”alisema
Madaraka ambaye alicheza naye Msamba Kajumulo WS na Simba SC.
Madaraka
alisema kwamba kwa sasa wanakusanyana rafiki zake ili kukutana na mke
wa marehemu kupanga taratibu za mazishi ya Msamba.
Msamba
ni mmoja kati ya washambuliaji bora wa pembeni kuwahi kutokea Tanzania
ambaye alikuwa ana nguvu, kasi na uwezo mkubwa wa kufunga mabao.
Kisoka
aliibukia Pan African pamoja na akina Bakari Malima, Thomas Mashalla,
Ally Yussuf ‘Tigana’ na wengineo kabla ya kuhamia Sigara na baadaye
Simba SC kisha kumalizia soka yake Kajumulo.
Mungu aiweke pema peponi roho ya marehemu. Amin.