come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

Tenga aishangaa serikali kuzikosesha Simba na Yanga kucheza Kagame


MWENYEKITI wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), Leodger Tenga, ameishukuru Serikali ya Tanzania kuziruhusu Simba na Yanga kushiriki Kombe la Kagame 2013, ingawa alikiri kuwa ridhaa hiyo imechelewa.


Tenga aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, alipozungumzia uamuzi wa Cecafa kuziba nafasi za Simba, Yanga na Falcon, zilizojitoa kutii agizo la serikali kutokana na hofu ya usalama mjini Darful, Sudan, ilikopangwa kufanyika michuano ya Kagame kuanzia Juni 18.

Aliongeza kuwa, usalama mashindanoni kwa namna moja si jukumu la Cecafa, bali serikali ya nchi mwenyeji, ambapo wao jukumu lao kubwa ni kupata bima (insurance), ambayo waliipata kutoka Serikali ya Sudan na kisha wao kuikabidhi wizarani baada ya serikali kuonesha shaka.

Alisema mchakato wa serikali kujiridhisha kwa kuipitia bima hiyo ulichukua muda, hivyo walipoamua kutoa ridhaa kwa timu zake, walikuwa wamechelewa, kwani licha ya timu kuvunja kambi, Cecafa ilishajaza nafasi hiyo kwa kualika timu nyingine.“Uamuzi wa Serikali ya Tanzania umetufariji sisi Cecafa, kwani umeondoa wingu zito la shaka kwa wadau wa soka wa ukanda huu, lakini pia umeisafisha Serikali ya Sudan ambayo ilituhakikishia usalama wa wachezaji mashindanoni,” alisema Tenga.

Aliongeza kuwa, Cecafa imekosa uwezo wa kuzirejesha Simba, Yanga na Falcon kutokana na uamuzi wa kuzialika URA ya Uganda, Rayon Sports ya Rwanda na Elect Sports ya Chad, kujaza nafasi hizo.“Kutokana na ukweli kuwa serikali ilizizuia klabu hizo, sisi tulijaza nafasi zao na kuzipa timu mbadala hadi tiketi za ndege na mahitaji mengine muhimu. Isingewezekana kuzitoa tena na kuzirejesha timu za Tanzania. Hivyo michuano itafanyika bila timu hizo,” alisema Tenga.

Akasisitiza kuwa, licha ya yeye kama Rais kutamani kuwaona mabingwa watetezi Yanga wakishiriki michuano hiyo, bado hakuna lililoharibika, kwani ushindani unaotarajiwa ni mkubwa, tena sawa na ule ambao ungepatikana kama zingekuwapo timu hizo.

Michuano ya Kagame inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Juni 18 na kufikia tamati Julai 2, katika viwanja vya Kadugl na El Fasher mjini Darful, jimbo linalosifika kwa mapigano ya waasi na Serikali ya Sudan, hali iliyozua hofu kwa serikali juu ya ukosefu wa amani.