Mzee huyo mwenye miaka 62, amefafanua kwamba lengo
lake si ugomvi na Simba bali anataka mambo yafanyike kisomi kwavile si
yeye aliyevunja mkataba uliokuwa umalizike Juni mwakani, bali ni Simba
ambayo ilimtumia barua pepe Mei 31 iliyovunja mkataba huo wa miezi 18.
“Kwa mujibu wa mkataba, yeyote kati yetu
atakayevunja mkataba atatakiwa kumlipa mwenzie fidia ya miezi miwili
mbele na kwavile wao ndio wamevunja wanapaswa kunilipa malimbikizo yangu
pamoja na fidia ambazo jumla ni dola 26,000 (Sh.41.5 milioni).
“Aprili nadai dola 2,000 sikulipwa mshahara wote,
Mei nadai mshahara mzima pamoja na Juni ambazo ni dola 12,000 na kwavile
wao ndio wamesitisha mkataba wanatakiwa kunilipa fidia ya dola 12,000
ambayo ni mishahara ya miezi miwili,” alisisitiza kocha huyo anayedai
hakuwahi kukaa meza moja ya majadiliano na Mwenyekiti wa Simba, Ismail
Aden Rage tangu Februari kwa maelezo kuwa bosi huyo yupo bize.
“Mimi nilitaka kumaliza muda wangu na Simba hata
kama wataniambia kwamba hawataongeza mkataba wangu, lakini tuachane kwa
amani. Mimi nimefanya kazi kwa shida sana Simba, lakini sikuwahi
kumwambia mtu kwavile naheshimu mkataba na najua siri za kazi, hakuna
aliyejua kwamba nilikuwa silipwi halafu naishi kwa shida hapa.
“Sikuwa na gari, vifaa vya kutosha, wachezaji
walikuwa na matatizo ya kila aina, mshahara wangu nilikuwa silipwi kwa
wakati sikuwa na nyumba wala ofisi niliishi hotelini muda wote, sasa
katika mazingira kama hayo kocha makini utafikiaje malengo? Lakini yote
hayo sikuwahi kusema nilikuwa naheshimu kazi,”aliongeza Liewig ambaye
kesho Jumapili atakutana na viongozi wa Simba.