Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, kocha wa Taifa Stars, Mdenmark Kim Poulsen alisema kuwa vijana wake wameiva na kwamba anaamini watawaduwaza mabingwa hao wa zamani wa Afrika (1992) na vinara wa viwango vya ubora wa soka barani.
Alisema kuwa wachezaji wake wanao uwezo na wanajua umuhimu wa kushinda mechi hiyo ambayo itaamua hatma ya Tanzania katika kampeni za kuwania kufuzu kwa fainali zijazo za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwakani nchini Brazil.
"Wachezaji wako katika hali nzuri kuelekea kwenye mechi hiyo, asubuhi (jana) tulifanya mazoezi na tutarejea tena jioni kujiandaa zaidi. Kesho (leo) tutapumzika hadi Jumamosi jioni (kesho) tutakapofanya mazoezi ya mwisho," alisema Poulsen.
"Tunajua mechi itakuwa ngumu kutokana na wapinzani wetu kuwa na uwezo mkubwa, lakini tunaamini tutawafunga kama tulivyofanya dhidi ya timu nyingine ngumu kama Zambia na Cameroon. Tunatambua umuhimu wa kupata ushindi katika mechi hiyo na hivyo tutapambana kufa na kupona," aliongeza Poulsen.
Tanzania na Ivory Coast zimepangwa Kundi C ambalo pia lina timu za Morocco na Gambia.
Ivory Coast ambao wanashika nafasi ya 13 katika orodha ya viwango vya ubora wa soka duniani, wanaongoza kundi hilo wakiwa na pointi 10, nne zaidi ya Stars inayoshika nafasi ya pili. Morocco wanaifuatia Stars wakiwa na pointi tano huku Gambia wakiwa mkiani mwa kundi hilo baada ya kuambulia pointi moja tu baada ya kushuka dimbani mara nne.
Taifa Stars, ambayo Jumamosi iliyopita ilikumbana na kipigo cha 2-1 dhidi ya mabingwa Afrika 1976, Morocco, itaingia uwanjani Jumapili ikiwa na kumbukumbu ya kufungwa ugenini 2-0 dhidi ya Ivory Coast katika mechi yao ya kwanza iliyochezwa Juni 2 mwaka jana kwenye Uwanja wa Félix Houphouët-Boigny mjini Abidjan.
Stars pia watahitaji kulipiza kisasi na kuendeleza ubabe kwa timu 'vigogo' barani Afrika zinazokuja kucheza nao kwenye Uwanja wa Taifa. Desemba 22 mwaka jana waliifunga Zambia 1-0, kisha wakaipa kipigo kama hicho Cameroon Februari 6 kabla ya kuiadhibu Morocco 3-1 katika mechi yao ya kwanza ya Kundi C la Kombe la Dunia iliyochezwa Machi 24 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.