Waziri mkuu wa Zimbabwe, Morgan Tsvangirai, ametoa taarifa muda mfupi tu baada ya agizo hilo la rais, akisema kuwa rais Mugabe amekiuka sheria kwa kutoshirikisha bunge na ameapa kupinga uamuzi huo.
Katika kikao na waandishi wa habari, Tsvangirai, amemshutumu Bwana Mugabe kwa kukiuka mkataba wa ugavi wa mamlaka uliosainiwa miaka mitano iliyopita, baada ya mzozo kuhusu matokeo ya kura kusababisha ghasia nchini humo.
Bunge la nchi hiyo bado linajadili mswada wa sheria ambao utaruhusu vyama vyote vya kisiasa kupewa nafasi sawa katika shirika la habari la serikali wakati wa kampeini.
Lakini wiki mbili zilizopita mahakama ya kikatiba nchini humo iliagiza kuwa uchaguzi huo ni sharti ufanyike kabla ya mwisho wa Julai.