come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

Yanga mbioni kumalizana na Kiiza

Mshambuliaji wa kimataifa wa Yanga, Hamis Kiiza
 
Mshambuliaji wa kimataifa wa Yanga, Hamis Kiiza, amesema kwamba yuko tayari kukaa msimu mzima bila ya timu lakini hataweza kushusha kiwango cha mshahara wa mwezi cha Dola za Marekani 3,500 (Sh. milioni 5.6) ambazo anataka mabingwa hao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara wamlipe kuanzia msimu ujao.

Kiiza alikuwa analipwa mshahara wa Dola za Marekani 1,500 kwa mwezi katika misimu miwili aliyoichezea Yanga baada ya kusainiwa kwa kiasi cha Dola za Marekani 30,000 na sasa ameitaka klabu hiyo iliyoutema ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) impe fedha ya kusaini Dola za Marekani 45,000 (Sh. milioni 72) ili asaini mkataba mpya.

Akizungumza  kwa njia ya simu kutoka kwao Kampala, Uganda, Kiiza alisema kuwa anaamini kiasi hicho cha fedha ndiyo kinalingana na thamani yake kwa sasa.

Mshambuliaji huyo ambaye yupo pia katika kikosi cha timu ya taifa ya Uganda (The Cranes) alisema kuwa mchezo wa soka ndiyo unaoendesha maisha yake na kwa kipindi hiki anatakiwa kufanya maamuzi sahihi ili aweze kujiandaa na maisha baada ya soka.

"Mimi kama nilivyowaambia sijabadilisha kitu, niko tayari hata kutorudi kama hawatakuwa tayari kunilipa, nami pia ninatoa mchango mkubwa kwa timu," alisema Mganda huyo.

Mbali na kiasi hicho cha mshahara ambacho kitakuwa ni cha juu ndani ya Yanga, Kiiza pia ameutaka uongozi umpatie nyumba ya kuishi na gari jipya la kutembelea akiwa hapa nchini.

Kiiza aliongeza kwamba licha ya kutofikia makubaliano na Yanga bado wakala wake hajampatia timu nyingine ya kwenda kufanya majaribio lakini wako kwenye mchakato huo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Abdallah Binkleb, aliliambia gazeti hili jana kwamba wao wako radhi kumuacha nyota huyo kama atashikilia msimamo wake huo.

Binkleb alisema kwamba wanaheshimu maamuzi yake kwa sababu wanajua ni kijana ambaye ana mipango na malengo yake kimaisha ambayo anataka kuyatimiza.

Kikosi cha Yanga kiko kwenye mapumziko na kinatarajia kuanza mazoezi upya Julai 2 mwaka huu kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa ligi utakaofanyika kuanzia Agosti 24.