come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

OPIYO AIPIGIA DEBE LEOPARDS

Peter Opiyo

Kiungo wa kati, Peter Opiyo, ameelezea imani yake kwamba klabu chake cha AFC Leopards kitakua kigezo kikuu katika harakati za kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Kenya.

Opiyo ameibuka kuwa nyota wa mabingwa hao wa zamani baada ya kujiunga nao kutoka watetezi wa taji hilo, Tusker, mwezi wa Juni.
Kufikia sasa, ameanza mechi mingi na alifungia Leopards bao lao la ushindi dhidi ya Sofapaka Jumapili.
Ushindi huo uliinua timu hiyo hadi nafasi ya tatu, ikitiliwa maanani kwamba walianza mkondo wa pili katika nafasi ya 11.
Hata hivyo, bado wako alama nane nyuma ya maasimu wao wa jadi na viongozi wa sasa, Gor Mahia ambao wana mechi moja ya ziada lakini, Opiyo haoni sababu ya kiwewe kutokana na mwanya huo mkubwa.
“Tuko katika hali mzuri na kikosi chetu kinacheza vyema zaidi. Nina furaha na shime kuu.
“Kupata bao la jana ni ajabu kwani lilitusaidia kushinda mechi muhimu. Tuko nafasi ya tatu karibu na kilele cha ligi na hapo ndipo tunastahili kuwa na tunatazamia kupanda zaidi kadri ya uwezo wetu.
“Ndio, Gor wana uongozi mkubwa lakini bado kuna mechi za kuchezwa na nina uhakika mwanya huo utapungua kwani bado watamenyana na vilabu kubwa na tutakuwa na fursa ya kuwakamata. Mradi tushinde mechi zetu,” mchezaji huyo alisema.
Leopards wamo alama moja nyuma ya Thika United ambao wanamiliki nafasi ya pili.