come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

JAVU ATAMBA KUNG'ARA LIGI MKUU YA TANZANIA BARA

Mshambuliaji mpya wa Yanga, Hussein Javu (Pichani) ametamka kuwa hatishwi na ushindani wa namba katika kikosi hicho ingawa anachukulia kama changamoto kutimiza malengo yake aliyojiwekea.

Kauli hiyo ya Javu imekuja baada ya hivi sasa kikosi cha Yanga kuwa na washambuliaji sita ambao watakuwa wakipigana nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza cha kocha Mdachi, Ernie Brandts katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani na kutetea taji la Ligi Kuu Bara msimu ujao.

Wachezaji hao ni Mrundi Didier Kavumbagu, Jerry Tegete, Said Bahanuzi, Shaban Kondo pamoja na Mrisho Ngassa.
Javu aliyesaini mkataba wa miaka miwili kukipiga na Yanga akitokea Mtibwa Sugar ya mjini Morogoro aliliambia gazeti hili jana jijini Dar es Salaam kuwa,”ushindani wa namba uko kila mahali, hata Mtibwa nilipotoka kulikuwa na ushindani wa kupata nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza.”
Alisema,”Naamini siwezi hata siku moja kujutia kujiunga na Yanga, nimekuja kwenye vita, kwa hiyo sina budi kupambana mpaka tone la mwisho, nafikiri haitakuwa rahisi kukubali kushindwa,” alisema Javu aliyezamisha mabao manane kwenye Ligi Kuu msimu uliopita.
Javu ambaye ana nguvu za kupambana na mabeki na kupiga mashuti yenye afya na kulenga lango la timu pinzani alisema,”Nafikiri ushindani kwangu nitauchukulia kama changamoto ya kutimiza malengo yangu niliyojiwekea ingawa naheshimu niliowakuta.”