ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Abdallah Bin Kleb, amerejeshwa tena katika uongozi wa timu hiyo na sasa anakuwa mjumbe wa Kamati ya Mashindano.
Bin Kleb aliondolewa Yanga hivi karibuni baada ya jina lake kutotangazwa na Mwenyekiti Yusuf Manji alipotaja wajumbe wa Kamati ya Utendaji na wengine kadhaa wanaounda kamati mbalimbali.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana Jumapili na Katibu Mkuu wa Yanga, Beno Njovu, Bin Kleb yupo kwenye kamati ndogo ya mashindano iliyoundwa na wajumbe wenza wa Kamati ya Utendaji ya Yanga (Maendelo ya Mchezo), Seif Ahmed ‘Seif Magari’ na Mhandisi Isaac Chanji.
Pia katika Kamati ya Ufundi iliyoundwa na wajumbe hao wapo, Nassoro Duduma, Roger Lamlembe, Pascal Malulu, Peter Msolla na Steve Zangira.
Kamati nyingine iliyotangazwa jana ni ile ya soka la vijana na wanawake, ambapo wapo Shaban Katwila, Jessica Kabisa, Isack Mazwile, George Mwita na Ally Mayay Tembele.
Baadhi ya wajumbe wengine wa Kamati ya Mashindano mbali ya Bin Kleb ni Magembe Cheyo, Ibrahim Didi, Ndama Hussein, Moses Katabalo, Mudhamiri Katunzi, Beda Tindwa na Lameck Nyambaya.
Chini ya kamati hizo, Yanga inatarajia kuwa na ufanisi mkubwa.