come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

MTANZANIA ATIA AIBU BBA, ATIMULIWA

Nando (Pichani), mmoja wa washiriki wawili wa Tanzania katika shindano la Big Brother Africa "The Chase", amefukuzwa katika shindano hilo baada ya kugombana na mwenzake Mghana Elikem (24) na kuhatarisha usalama wake kwa kwenda kitandani na mkasi, siku chache baada ya kwenda kwenye "pati" ya BBA akiwa na kisu.
Kijana huyo ambaye aliingia BBA kuiwakilisha Tanzania akitokea Marekani anakoishi, amefukuzwa kwa kuvunja kanuni za usalama wakati alipogombana na kijana huyo wa Ghana mwenye mwili mkubwa uliojengeka kimazoezi.

Kabla ya kufukuzwa, Nando alipewa maonyo matatu, ambayo Big Brother alishawaeleza washiriki mapema kwamba atakayeonywa mara tatu atakuwa ameenguliwa moja kwa moja mchezoni. Onyo la kwanza lilikuja katika wiki ya tano mjengoni baada kubeba kisu kwenye sherehe ya Big Brother.

Kufuatia kugombana na Elikem Ijumaa usiku, Big Brother alimpa maonyo mengine mawili, moja kwa kufanya fujo na jingine kwa kuficha mkasi kitandani mwake kufuatia ugomvi wake na Elikem, hivyo kukamilisha maonyo matatu yanayomfukuza mshiriki moja kwa moja.

Kutokana na ushiriki wake katika ugomvi huo, Elikem alipewa onyo la kwanza na Big Brother.

Tanzania sasa imebakiwa na mshiriki mmoja, kimwana Feza Kessy (25) katika shindano hilo linaloelekea ukingoni likiwa limebakiwa na jumla ya washiriki tisa tu katika ya 28 walioanza mbio za kuwania zawadi ya mshindi wa mwaka huu ambayo ni dola 300,000 (Sh. milioni 485).

Tanzania ndiyo iliyokuwa nchi pekee iliyobaki na wawakilishi mjengoni humo kutoka Afrika Mashariki baada ya kimwana Annabel wa Kenya kuaga juzi na kufanya nchi za Kenya na Uganda kukosa washiriki. Kila nchi ilikuwa na wawakilishi wawili.

Nando, ambaye wakati akiingia katika shindano hilo alisema alikuwa hajawahi kuangalia shoo ya Big Brother Afrika, alisema alishawishiwa na rafiki zake kuingia katika shindano hilo.

Akiwa mjengoni, Nando ambaye alisema anapenda kuangalia kipindi cha televisheni cha "1000 Ways To Die", alikuwa amepanga baada ya shindano hilo ashirikiane na Feza kuwasaidia kaka zao wa damu ambao walidai ni 'wateja' wa dawa za kulevya. Feza alisema mdogo wake wa kiume mwenye umri wa miaka 23 amekuwa ni mteja dawa za kulevya za 'heroin' kwa miaka saba iliyopita na akaongeza pia kwamba mdogo wa Nando pia ni 'mteja' wa dawa za kulevya za heroin ambaye ametoweka kwao.