come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

BIN KLEB AITULIZA YANGA KUHUSU KIIZA

Kamati ya usajili ya klabu ya Yanga ya jijini Dar es Salaam imesema kwamba bado inaendelea 'kuvutana' na mshambuliaji wao wa kimataifa, Mganda Hamis Kiiza ili akubali kusaini mkataba mpya wa kuitumikia timu hiyo inayoshikilia ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

Akizungumza jana kwenye makao makuu yao yaliyopo katika mitaa ya Twiga na Jangwani, Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano na Usajili ya Yanga, Abdallah Binkleb  (Pichani), alisema kuwa hadi jana walikuwa bado hawajakamilisha mazungumzo na mchezaji huyo ambaye kocha wao, Ernie Brandts ameshasema kuwa anamuhitaji sana aendelee kuwapo kwenye kikosi chake.

Binkleb alisema kuwa bado Yanga haijatoa maamuzi ya kumpa mchezaji huyo mahitaji yote aliyoyataka na hiyo inatokana na mapendekezo ya Kiiza kuzidi bajeti waliyoitenga kwa ajili ya mshambuliaji huyo ambaye pia anaichezea timu ya taifa ya Uganda (The Uganda).

"Bado hajasaini hadi leo (jana), hatujafikia makubaliano kuhusiana na vitu ambavyo ametaka apatiwe ili asaini," alisema Binkleb.

Hata hivyo, Binkleb aliongeza kuwa bado wanaendelea vyema na mazungumzo na hiyo inaonyesha kuwa pande zote mbili zina nia njema ya kufikia maridhiano kabla ya kuanza kwa msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

Alisema kuwa hivi sasa mshambuliaji huyo aliyeichezea Yanga kwa mafanikio makubwa katika misimu miwili yupo na familia yake nyumbani kwao Uganda.

Kiiza ameiambia Yanga kuwa hayuko tayari kusaini mkataba mpya hadi alipwe kwa mkupuo dola za Marekani 40,000 (Sh. milioni 65) pia awe akilipwa mshahara wa kila mwezi wa dola za Marekani 1,500 (Sh. milioni 2.4).

Nyota huyo pia anadaiwa kutaka alipiwe nyumba ya kuishi na gari la kutembelea ambalo thamani yake iwe walau Sh. milioni 10.

Wachezaji wengine wa kigeni waliosajiliwa Yanga ni pamoja na kiungo kutoka Rwanda, Haruna Niyonzima 'Fabregas' na mshambualiji raia wa Burundi, Didier Kavumbagu.

Yanga inaendelea na mazoezi yake kwa ajili ya msimu ujao ambapo Agosti 17 watazindua msimu mpya wa ligi kwa kuivaa Azam katika mchezo wa kuwania Ngao ya Jamii na Agosti 24 wataanza ligi kwa kucheza mechi yao ya ufunguzi dhidi ya timu iliyorejea ligi kuu ya Ashanti ya Ilala.