Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Poulsen alisema anachoamini kuwa kutolewa kwao katika mashindano hayo kulitokana na makosa ya kiufundi, lakini si kwa sababu ya ubovu wa kikosi alicho nacho.
Poulsen alisema kuwa bado kikosi hicho kinajengwa, ingawa waliamini kwamba walau wangeweza kuifunga Uganda na kusonga mbele kwenye michuano ya CHAN.
Alieleza kwamba kutolewa kwao na wapinzani wao Uganda (The Cranes), kulitokana na makosa ya kiufundi, hasa pale wachezaji wake waliporuhusu goli la pili na la tatu kufungwa, hivyo wakajikuta wakiondolewa mchezoni na kuwapa nafasi wenyeji kuwabana.
"Ninaiamini timu yangu, bado ni timu nzuri... kufungwa kwetu ni moja ya makosa ya kimchezo na hivyo siwezi kuwalaumu sana wachezaji. Hakikuwa kikosi kibaya," alisema Kim ambaye awali alikuja nchini na kupewa kibarua cha kufundisha timu ya taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 (U-20) kabla ya kupandishwa baadaye kufuatia kuondoshwa kwa mtangulizi wake, raia mwenzake wa Denmark, Jan Poulsen.
Poulsen aliongeza kuwa hivi sasa anajipanga kwa ajili ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa mwaka 2015 huku akisema kwamba Stars itarejea tena kambini ifikapo Agosti 29 kujiandaa na mechi ya ugenini dhidi ya Gambia ambayo ni ya kukamilisha ratiba ya Kundi C la mechi za kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia.
Stars ilirejesha nchini juzi ikitokea Kampala ambapo iliiaga michuano ya CHAN baada ya kupata kipigo cha jumla cha magoli 4-1 kutoka kwa Uganda; wakikubali kipigo cha nyumbani cha 2-1 wiki mbili zilizopita na juzi kuchapwa tena kwa mabao 3-1.