Mashabiki wa Yanga walisubiri hadi dakika ya 90,
wakati mshambuliaji Jerryson Tegete alipofunga bao la kusawazisha baada
ya mabeki wa URA kushindwa kuelewana na kipa wao.
Mshambuliaji wa URA , Lutimba Yayo aliifungia timu
yake mabao mawili ya kuongoza katika dakika 42 na 51, kabla ya Didier
Kavumbagu kuipatia Yanga bao katika dakika ya 66 na Tegete kuisawazishia
Yanga.
URA walitawala vizuri kipindi cha kwanza ikiwa ni
saa 24, tangu walipoichapa Simba kwa mabao 2-1 kwenye uwanja huo. Katika
dakika ya 4, Derrick Walulya nusura aifungie timu yake bao baada ya
shuti lake kupaa juu kidogo ya goli la Yanga.
Kipa mpya wa Yanga, Deogratias Munish ‘Dida’
alithibitisha ubora wake baada ya kuokoa shuti la Ngama Emmanuel akiwa
ndani ya eneo la 18 katika dakika ya 27.
Yanga walimtoa Hamis Thabit na kumwingiza Bakari
Masoud katika dakika 40, wakati URA waliwapumzisha, Joseph Owino, Ngama
Emmanuel na kuwaingiza Munaaba Allan na Ike Obina.
Dakika tatu kabla ya mapumziko URA walipata bao la
kuongoza lililofungwa na Yayo kwa shuti kali baada ya kuwazidi ujanja
mabeki wa Yanga.
Waganda walirudi kipindi cha pili kwa nguvu zaidi
na kufanikiwa kupata bao la pili lilililofungwa na Yayo kwa shuti la
mpira wa adhabu baada ya beki wa Yanga, Ibrahimu Job kumchezea vibaya
Ngama Emmanuel katika dakika 51.
Mshambuliaji Kavumbagu alifungia Yanga bao la
kwanza katika dakika 66, akiuganisha kwa kichwa krosi ya Juma Abdallah.
Kocha wa Yanga, Ernest Brandts alimtoa Bahanuzi na kumwingiza Haruna
Niyonzima katika dakika 77, ambapo mabadiliko hayo yalikuwa na faida
kwa Yanga kwani iliwasaidia kurudi mchezoni.