Kiongozi wa zamani wa upinzani nchini Burundi Agathon Rwasa anarejea nyumbani baada ya miaka mitatu ya kuwa nje ya nchi.
Rwasa alikua kiongozi wa chama cha FNL lakini alipokonywa uongozi baada ya kutoroka nchi akihofia maisha yake.
Mwanasiasa huyo aliondoka Burundi baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, alipolalamikia kwamba uchaguzi huo haukuwa huru na wa haki.
Umoja wa Mataifa umekua ukiwasihi wanasiasa wa Burundi waliokimbia nchi, kurejea nyumbani kama hatua ya kuondoa taharuki za kisiasa.
Hata hivyo serikali ya Pierre Nkurunzinza imekuwa ikimuona Rwasa kama tisho la kisiasa tangu kutoroka nchi hiyo, ingawa Rwasa alirejea mjini Bujumbura kwa shangwe na vigelegele kutoka kwa wafuasi wake baada ya kuhakikishiwa usalama wake.
Rwasa anatarajiwa kukutana na wafuasi wake katika kile upande wake unasema ni kuwapatanisha kabla ya uchaguzi mkuu mwaka 2015, kwa sababu ananuia kuwania urais dhidi ya rais Pierre Nkurunzinza.
Rwasa, ambaye alikuwa mapinzani mkuu wa rais Pierre Nkurunziza wakati wa uchaguzi wa mwaka 2010 , alisema alihofia maisha yake na hivyo kurejea msituni mwezi Juni mwaka huo.
Hata hivyo hali yake haikujulikana tangu hapo, huku baadhi ya ripoti zikisema kuwa alionekana mpakani katika mkoa wa Kivu Kusini katika Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo, nchini Tanzania na Zambia.
Upande wa Rwasa ulikanusha kuwa aliwahi kutoroka Burundi.
Burundi nchi ambayo ilikumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe ingali inakumbwa na athari za vita hivyo vilivyosababisha vifo vya watu laki tatu kati ya mwaka1993 na 2006.
Serikali imelaumu chama cha FNL kwa mashambulizi ya mara kwa mara ya kuvizia huku kukiwa na madai kuwa Rwasa alikuwa anaanzisha tena uasi dhidi ya serikali