come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

NGASA AJIPA MATUMAINI KIBAO, AWATAKA MASHABIKI YANGA KUTULIA

Mshambuliaji wa Yanga, Mrisho Ngassa (Pichani), amesema kuwa hana hofu na adhabu ya kufungiwa aliyopewa na Kamati ya Sheria, Katiba na Hadhi za Wachezaji na kuwataka mashabiki wa timu hiyo kujiandaa kumuona uwanjani hivi karibuni.


Ngasa amefungiwa kucheza mechi sita pamoja na kutakiwa kuilipa Simba Sh. milioni 45 kutokana na kamati hiyo kutambua mkataba wa mwaka mmoja aliousaini mwaka jana wakati akijiunga na klabu hiyo akitokea Azam.

Kamati hiyo ilieleza kuwa mchezaji huyo hataruhusiwa kuanza kucheza hadi atakapolipa kiasi hicho cha fedha.

Akizungumza  jana, Ngasa alisema kuwa suala hilo  amewaachia viongozi wake na anaamini wakati anajiunga na Yanga walipata ushauri wa kisheria kabla ya kumpa mkataba mwingine baada ya msimu wa ligi kumalizika Mei mwaka huu.

Ngassa alisema kuhalalishwa Yanga ndiyo iliyokuwa ndoto yake na sasa imetimia.
"Bado sijaambiwa kitu chochote, najua viongozi watalifanyia kazi ili niweze kurudi uwanjani mapema, mechi sita...sidhani kama nitakaa nje muda wote," alisema kwa kifupi mshambuliaji huyo ambaye aliwahi pia kuichezea Kagera Sugar ya Bukoba.

Hata hivyo, Ngasa alikataa kuelezea mkataba aliousaini Simba mwaka jana huku akiongeza mambo yanayohusu mikataba ni ya baina ya pande mbili zilizoingia makubaliano.

Mshambuliaji huyo tegemeo pia katika kikosi cha timu ya Taifa (Taifa Stars) mwaka jana alikataa ofa ya kujiunga na klabu ya El Mereikh ya Sudan licha kuahidiwa donge nono pamoja na mshahara wa juu ukilinganisha na anaopewa na mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Yanga.

Ngassa alianza kuitumikia adhabu hiyo Jumamosi wakati alipoishuhudia kutokea jukwaani timu yake ya Yanga ikitwaa Ngao ya Jamii kwa kuifunga Azam 1-0 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Wakati huo huo, habari kutoka ndani ya Yanga zinasema kwamba wako katika hatua za mwisho za kuwasilisha malalamiko yao katika Kamati ya Nidhamu kupinga adhabu hiyo iliyotolewa kwa mchezaji wao.