Kenya imesaini mkataba na China
ambao unatoa dola bilioni tano kuimarisha huduma za Reli,Kawi na
Uhifadhi wa Wanyama Pori kwa taifa hilo la Afrika Mashariki.Makubaliano
hayo yaliafikiwa katika ziara ya Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta nchini
China.
Hii ndio ziara ya kwanza ya Rais Kenyatta tangu kuchaguliwa hapo mwezi Machi mwaka huu.Serikali ya Kenya imepongeza mkataba huo na kusema utasaidia nchi kukua kiuchumi na kuboresha maisha ya raia wake.
Mwenyeji wa Kenyatta, Rais wa ChinaXi Jinping , ameelezea kuridhishwa kwake na juhudi za serikali ya Bw Kenyatta katika kuimarisha taifa la Kenya.
Uhusiano kati ya Uhuru Kenyatta na dola za magharibi umedorora kufuatia mashtaka dhidi yake katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita-ICC. Kenyatta anatarajiwa kwanza kesi dhidi yake baadaye mwaka huu.
Ametuhumiwa kwa kufadhili ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007, japo amekanusha madai hayo. Wakati wa kampeini za uchaguzi mkuu nchini Kenya Muungano wa Ulaya ukitishia kupuuza Kenyatta endapo angechaguliwa Rais.
Nayo Marekani ilionya Wakenya dhidi ya kuwachagua washukiwa wa dhuluma za kivita.
Bw. Kenyatta amelaani dola za Magharibi kwa kile alichokitaja kama mwingilio wa masuala ya ndani ya nchi.
Mmoja wa miradi inayotarajiwa kuimarishwa ni huduma ya reli itakayounganisha bandari ya Mombasa na Mji wa Malaba ulioko mpaka na Uganda.
China pia inatarajia kufadhili miradi ya kilimo, mbolea na teknolojia nchini Kenya.