Mkuu wa ujumbe wa uangalizi
kutoka Muungano wa Afrika nchini Zimbabwe, Olusegun Obasanjo amesema
uchaguzi mkuu wa hapo Jumatano ulikua huru na haki. Matokeo ya awali
yanaoyesha Rais Robert Mugabe na chama tawala cha Zanu PF wakiongoza kwa
kura nyingi
Lakini mpinzani wa Mugabe, Morgan Tsvangirai, amesema uchaguzi huo ni wa uongo na kusema udanganyifu uliofanyika una maana uchaguzi huo haukubaliki.
Waangalizi kutoka Umoja wa Afrika na jumuia ya maendeleo kusini mwa Afrika wanatarajiwa kutoa tamko rasmi hii leo kuhusu uchaguzi huo.
Bw. Obasanjo amesema kulikua na visa kadhaa wakati wa shughuli ya kupiga kura. Hata hivyo amesema visa hivyo haviwezi kutajwa kuwa na uzito wa kubatilisha au kufuta matokeo ya kura.
Msimamo wa Muungano wa Afrika unatofautiana na ule wa kundi la uangalizi la Zimbabwe Election Support Network.
Kundi hilo ambalo ndilo kubwa zaidi linalochunguza kura ya Zimbabwe limekashifu uchaguzi mkuu na kusema ulikuwa na dosari nyingi. Hii ni kwa sababu watu milioni moja walizuiwa kupiga kura.
Huku upande wa Rais Mugabe ulitangaza kushinda uchaguzi na Morgan Tsvangirai akipinga ni dhahiri kwamba Zimbabwe ingali na mgawanyiko mkubwa wa kisiasa..