MSANII wa muziki wa kizazi kipya nchini, Omary Nyembo ‘Ommy Dimpoz’ (Pichani) anajipanga kuachia albamu yake ya kwanza ambayo bado hajaipa jina kutokana na ubora wa nyimbo zilizomo ndani yake.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Meneja wa msanii huyo, Mbarouk Issa ‘Mubenga’, alisema, msanii huyo yupo katika maandalizi ya albamu hiyo, ambayo itakuwa na nyimbo kadhaa ambazo zimefanya vizuri katika soko hilo.
“Kwa sasa yupo katika maandalizi ya albamu hiyo, naomba wapenzi wake wakae mkao wa kula kwa ajili ya kazi hii, ambayo naamini itakuwa na burudani iliyokamilika kutokana na mashairi ya nyimbo hizo kusimama,” alisema.
Dimpoz kwa sasa anatamba na kazi yake inayokwenda kwa jina la ‘Tupogo’, ambayo amemshirikisha mkali kutoka Nigeria, J. Martins.
Mbali na ‘Tupogo’, msanii huyo alikwishawahi kutamba na kazi zake za ‘Nai nai’, ‘Baadaye’, ‘Me and You’ na nyinginezo.