SAKATA la Klabu ya Yanga kugomea haki za mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara kumilikiwa na Azam TV jana lilipata ufumbuzi kupitia kikao kilichoitishwa na Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makala, dhidi ya pande husika.
Kuitishwa kwa kikao hicho ni baada ya Yanga chini ya Mwenyekiti wake, Yusuf Manji, kuomba serikali kuingilia kwa hoja mbalimbali, ikiwamo klabu kutoshirikishwa vya kutosha katika mchakato huo ulioipa Azam TV idhini ya kuhodhi haki za ligi hiyo.
Akizungumza baada ya kikao hicho kilichodumu kwa saa mbili, Mwenyekiti wa Kamati ya Ligi, Wallace Karia, alisema wanashukuru kikao kilikwisha vizuri na hakuna mshindi wala mshindwa, kwani mchakato wa udhamini huo utaendelea huku hoja za Yanga zikifanyiwa kazi.
“Tunashukuru Mungu kikao chetu kimekwenda vizuri sana, niseme hakuna mshindi wala mshindwa, kwa sababu tumekubaliana kuwa mchakato wa Azam TV uendelee na hoja za Yanga zikizingatiwa kwenye mchakato wenyewe, kuhakikisha unakuwa ni mkataba wenye masilahi kwa klabu,” alisema Karia.
Karia alisema uamuzi huo ulifikiwa baada ya Yanga kuwasilisha hoja zao na pande nyingine pia kufanya hivyo, hivyo wakajadili kwa kina na kufikia uamuzi huo, kwamba mchakato wa Azam TV uendelee kwa vile hata mkataba husika unaweza kusainiwa baada ya Agosti 25.
Alisema Yanga kwa upande wao wameomba wawe na mwanasheria wao kuhakikisha masilahi yao yanazingatiwa kwenye mkataba huo, jambo ambalo lilikubaliwa na pande zote, Kamati ya Ligi na Azam TV.
“Kwa masilahi ya soka, hilo la Yanga kuwa na mwanasheria wake tumelikubali na upande wa Azam TV wamelipokea na wapo tayari hata kwa mazungumzo na Yanga kuangalia ni kwa namna gani masilahi kulingana na hadhi yao yatazingatiwa,” alisema Karia.
Alisema Azam TV wapo tayari kuipatia klabu hiyo mkataba binafsi kama ilivyo kwa watani wao Simba, kwani lengo ni kuhakikisha soka ya Tanzania inapiga hatua.