Mji mkuu wa Misri Cairo umeripotiwa kuwa kimya, baada ya operesheni ya kinyama dhidi ya waandamanaji wanaomuunga mkono rais aliyepinduliwa Mohammed Morsi kupelekea vifo vya mamia ya raia. Mauaji hayo yamezua shutuma kutoka jamii ya kimataifa.
Zaidi ya watu 278 waliuwawa wakati maafisa wa usalama waliposhambulia kambi mbili za wafuasi wa Bwana Morsi. Kambi hizo zilianzishwa mwezi uliopita kupinga hatua ya jeshi kumng'oa rais huyo anayezingatia itikadi za kiislamu.
Hali ya hatari imetangazwa na amri ya kutotoka nje nyakati za usiku kutolewa katika miji mikuu ya Misri.
Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa marekani John Kerry amesema matukio ''mabaya'' yaliyotokea ni ''pigo kubwa kwa juhudi za maridhiano''.
Afisa wa mashauri ya kigeni katika Muungano wa Ulaya, EU, Catherine Ashton na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon kadhalika wamekosoa hatua ya maafisa wa usalama kutumia nguvu dhidi ya raia.
Raia wa Misri wanaamkia siku nyingine yenye shaka juu ya mustakabal wao, anasema mwandishi wa BBC Bethany Bell aliyepo mjini Cairo.
Hata baada ya amri ya kutotoka nje kuondolewa Alhamisi asubuhi, kumekuwa na magari machache katika barabara za katikati mwa Cairo na madaraja yanayovuka mto Nile, anasema mwandishi wetu.
'Pigo kubwa'
Waandamanaji wamekuwa wakiitisha bwana Morsi aliyetimuliwa na jeshi tarehe 3 Julai, kurejeshwa madarakani.
Vuguvugu la undugu wa Kiislamu, Muslim Brotherhood, ambalo lilifadhili maandamano ya hivi punde katika medani ya Nahda na pia karibu na muskiti wa Rabaa al-Adawiya, limesema kuwa idadi ya kweli ya watu waliouwawa siku ya Jumatano inazidi 2,000.
Kwa mujibu wa serikali ya mpito inayoungwa mkono na jeshi, raia 235 waliuwawa kote nchini, pamoja na maafisa wa polisi 43. Tarakimu hizi haziwezi kuthibitishwa kwa njia iliyo huru.
Bwana Kerry amesema juhudi za maridhiano ya kisiasa nchini Misri zimepata "pigo kubwa".
"Hii ni hatua muhimu kwa Wamisri wote," akaongeza bwana Kerry. " Mkondo wa vurugu utaelekea tu kwa msukosuko zaidi, mkasa wa kiuchumi na mateso."
Afisi ya katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon imesema kuwa ''anasikitika kwamba maafisa wa Misri waliamua kutumia mabavu wakati Wamisri wengi wanataka taifa lao kusonga mbele kwa amani katika mfumo utakaoongozwa na Wamisri wenyewe ili kuafikia maendeleo na demokrasia".
"Akilaani vikali" vurugu zilitokea Bi. Ashton amesema kuwa " ni juhudi za pamoja pekee kati ya Wamisri wote pamoja na jamii ya kimataifa ndizo zitakazorejesha taifa hilo katika demokrasia inayowashirikisha wote na kukabili changamoto zinazokabili Misri".