Ngassa alisema kwamba yeye anaamini fedha kiasi cha Sh. milioni 30 na gari alilopewa na viongozi wa Simba ilikuwa ni kwa ajili ya kukubali kuhamia katika timu hiyo kwa mkopo.
"Ninachojua mimi niko Yanga, mengine watamalizana wenyewe," alisema mshambuliaji huyo ambaye aliwahi pia kuichezea Kagera Sugar ya mjini Bukoba.
Afisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema jana kuwa kikao cha kamati hiyo chini ya mwenyekiti Alex Mgongolwa, kilishindwa kukaa juzi na jana kama ilivyopangwa kutokana na wajumbe wa kamati hiyo kutofikia idadi inayotakiwa.
Wambura alisema kwamba hivi sasa, tayari mawasiliano yamefanyika na wajumbe wote wameahidi kuwapo kesho ili kupitia usajili huo na kutangaza maamuzi yao ikiwa ni siku moja kabla ya mechi ya kuwania Ngao ya Jamii kati ya Yanga na Azam.
"Kamati hiyo sasa itakutana Ijumaa (kesho) saa 4:00 asubuhi kupitia usajili huo. Maamuzi yote yatatangazwa siku hiyo," alisema Wambura.
Alisema kuwa kamati hiyo ina wajumbe saba na ili kikao kifanyike, ni lazima idadi yao ifikie walau watu wanne ili mwishowe maamuzi yao yatatambuliwa.