KWA mara ya pili leo, mshambuliaji wa Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’, Mbwana Ally Samatta amekuwa mchezaji bora wa mechi ya kusaka mshindi wa tatu wa Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challengedhidi ya Zambia, iliyoshinda kwa penalti 6-5 kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 90.
Samatta awali alikuwa mchezaji bora wa mechi kati ya Kili Stars na Uganda ‘The Cranes’ ya Robo Fainali ya CECAFA Challenge, siku hiyo akipika mabao yote mawili yaliyofungwa na Mrisho Ngassa timu yake ikitoka sare ya 2-2 ndani ya dakika 90 kabla ya kushinda kwa penalti 3-2.
Na leo Mbwana baada ya kuifungia Stars bao la kusawaisha na kufunga penalti ya kwanza, amepewa tena heshima ya mchezaji bora wa mechi, inayoambatana na zawadi ya king’amuzi na kifurushi kutoka GOtv
Kipa Ivo Mapunda alipangua penalti mbili za Wazambia, Justin Zulu na Kondwani Mtonga, lakini Haroun Chanongo, Mrisho Ngassa na Nahodha Kevin Yondan wote wakakosa penalti zao zikiokolewa na kipa wa Chipolopolo, Joshua Titima.
Waliofunga penalti za Zambia ni Felix Katongo, Ronald Kampamba, Bronson Chama, Julius Situmbeko, Rodrick Kabwe na Kabaso Chongo, wakati za Stars zilifungwa na Mbwana Samatta, Erasto Nyoni, Himid Mao, Amri Kiemba na Ramadhani Singano ‘Messi’.
Katika mchezo huo, Zambia walitangulia kupata bao dakika ya 52 kupitia kwa Ronald Kampamba kabla ya Mbwana Samatta kufunga bao zuri mno dakika ya 65 akiisawazishia Stars.
Mchezo huo ulisimama kwa dakika sita, dakika ya 88 kufuatia Polisi kufyatua mabomu ya machozi wakipambana na mashabiki wa Kenya waliokuwa wanataka kuingia bure uwanjani.
Wachezaji walianza kuanguka mmoja mmoja kutokana na kuzidiwa na hewa ya mabomu, hivyo marefa wakasimamisha mchezo kabla ya kuanza tena dakika sita baadaye.
Kwa matokeo hayo, Stars inaondoka Challenge ya 2013 na nafasi ya nne kama mwaka jana mjini Kampala, Uganda ilipofungwa kwa penalti pia na Zanzibar katika mchezo wa kusaka mshindi wa tatu.