Tanganyika ilipata uhuru wake kutoka kwa wakoloni wa Kiingereza Desemba 9, mwaka 1961.
Katika maadhimisho hayo, mbali na karibu asilimia 90 ya hotuba ya Rais Kikwete kumzungumzia marehemu Mandela, aliamuru kusitishwa kwa shamrashamra za ngoma za asili kama ilivyozoeleka na badala yake ilikuwapo halaiki pekee.
“Kutokana na kuomboleza kifo cha Mandela, leo hatutakuwa na watu wa ngoma za asili. Nimeongea na walioandaa sherehe hizi na tumekubaliana kuwa watu wa ngoma watatumbuiza kipindi kingine,” alisema Rais Kikwete.
Mandela alifariki dunia nyumbani kwake Johannesburg, Afrika Kusini baada ya kusumbuliwa na maradhi ya mapafu kwa kipindi kirefu. Anatarajiwa kuzikwa katika kijiji alichokulia cha Qunu Jumapili ijayo.
Katika hotuba yake iliyochukua dakika 25, huku akitumia jina la ‘mtu muungwana’, Rais Kikwete alisema Mandela alikubali kusamehe na kukaa meza moja na wabaya wake.
Alisema licha ya kufungwa gerezani na kuteswa kwa kipindi cha miaka 27, aliporejea uraiani alionyesha moyo wa huruma na kuwasamehe waliomtesa.
“Kwa kawaida siku kama ya leo siyo ya kutoa hotuba, lakini kutokana na tukio kubwa tulilonalo, ningependa niseme machache kuhusu Mandela.
“Mandela alikuwa mtu wa aina yake na itatuchukua miaka mingi duniani kumpata kiongozi kama huyu. Alikuwa muungwana na kuwashangaza wengi kuanzia wale waliomtesa hata wale walioteswa. Alikubali kusamehe na hakutaka kulipiza kisasi.”
“Hapa najua tupo wengi tunaojiandaa kulipa kisasi, tunatakiwa kujifunza kwa Nelson Mandela.
Heshima aliyojijengea leo hii ndiyo inayosababisha mazishi yake kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwamo kutoka mataifa makubwa,” alisema.
Rais Kikwete alisema Mandela alikuwa kiongozi aliyeamini katika ukweli na wakati wote alipigania haki na uhuru wa watu weusi walionyanyaswa na kuteswa katika ardhi yao na kwamba daima alisimamia ukweli hata kama msimamo wake ulihatarisha maisha yake.