MSHAMBULIAJI Luis Suarez amethibitisha hataondoka Liverpool katika dirisha dogo— na amesema Ligi Kuu England ni bora duniani.
Lakini bado anagoma kuongeza Mkataba na klabu hiyo ya Anfield.
Real Madrid imekuwa ikihusishwa na kumnunua mchezaji huyo wa Uruguay ifikapo January ili akakate kiu yake ya kucheza Ligi ya Mabingwa.
Lakini bada ya kufunga mabao manne kattika ushindi dhidi ya Norwich jana aliliambia gazeti la Marca: "Ninapokuwa nina furaha nje ya Uwanja; inaonyeshwa na kiwango changu uwanjani. Nina furaha katika Ligi Kuu ya England; ni ambako kuna ligi bora,".
Alipoulizwa kama atabaki hadi mwishoni mwa msimu unaoendelea, alisema: "Ndiyo, nina furaha hapa na nitabaki,".
Suarez sasa anaongoza kwa mabao katika Ligi Kuu ya England, akiwa amefunga mara 13 licha ya kukosa mechi tano za mwanzo akitumikia adhabu.
"Bahati nzuri nafunga mabao kufidia mechi nilizokosa. Ninapata hali ya kujiamini kuweza kuisaidia zaidi timu. Kitu cha msingi ni kufuzu Ligi ya Mabingwa baada ya muda mrefu ya kuwa nje ya nne bora. Nataka kuisaidia timu kufikia mafanikio hayo,".
Licha ya kuonyesha kiwango cha juu, mshambuliaji huyo wa Liverpool amesema kwamba anabaki kuwa chini ya Leo Messi na Cristiano Ronaldo.
Alipoulizwa kuhusu tuzo ya Mwanasoka Bora wa Dunia wa FIFA, alisema: "Ballon d’Or ni haiwezekani kwangu, nyota wengine wakiwania tuzo hiyo. Wako katika kiwango kingine,".