Akiwa amebakiza siku 10 kabla ya mkataba wake na mabingwa wapya wa Ligi Kuu ya Soka ya Kenya, Gor Mahia, kipa chaguo la kwanza kwa Kilimanjaro Stars, Ivo Mapunda, amesema hakuna timu yoyote mpaka sasa iliyomfuata kwa ajili ya kufanya mazungumzo ya kumsajili.
Mapunda alisema yuko tayari kuichezea timu yoyote itakayomhitaji kwa sababu soka ndiyo kazi yake.
Kipa huyo wa zamani ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Yanga na Prisons ya Mbeya, alisema anaamini kiwango chake kiko juu na hatakosa klabu ya kuichezea hapo mwakani.
"Niko huru, sijafanya mazungumzo rasmi na klabu yoyote ya nyumbani (Tanzania) au hapa Kenya, hata mabosi wangu wa Gor Mahia bado sijazungumza nao," alisema Ivo ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika Desemba 16, mwaka huu.
Mapunda alisema pia licha ya kuwa na kiwango cha juu, lakini anaheshimu maamuzi ya Kocha Mkuu wa Gor Mahia, Bobby Williamson, kumuweka benchi mara kwa mara.
"Kila siku unatakiwa ukubaliane na maamuzi ya makocha, ila naamini mimi niko juu licha ya kuonekana ni kipa namba mbili katika timu yangu kwa sasa," Mapunda aliongeza.
Mmoja wa wadau wa soka wa Kenya, Timoth Obolulu, alisema kiwango cha Mapunda kimezidi kuimarika na klabu yoyote itakayomuhitaji kwa sasa inatakiwa ijipange kwa kujiandaa kutoa dau la juu.