come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

MAKALAUENDAWAZIMU GANI HUU KUUZA WACHEZAJI BILA PESA

Na Prince Hoza

WANASEMA ukiyastaajabu ya Mussa utayaona ya Firauni, msemo huo umeendelea kubakia midomoni mwa wengi na kikubwa yanapotokea mambo ya kushangaza, sakata la usajili wa mshambuliaji Emmanuel Okwi limemalizika rasmi.

Sakata hilo lilitawala vyombo vya habari ambapo kila kukicha habari ni za Okwi, Okwi alizua utata baada ya kusajiliwa na mabingwa wa soka nchini Yanga akitokea SC Villa ya Uganda.

Kitu cha kushangaza kuwa SC Villa ilipewa tu kwa kibali maalum na shirikisho la kandanda ulimwenguni Fifa, kibali hicho kiliruhusu Okwi kuichezea SC Villa kwa miezi sita kufuatia mgogoro kati ya Okwi na klabu yake ya Etoile Du Sahel ya Tunisia ambayo ilimnunua toka klabu ya Simba ya Tanzania.

Uhamisho wa Okwi toka Simba kwenda Etoile Du sahel uliibua maswali mengi yaliyokosa majibu, kilichopelekea kuibua maswali ni kwamba klabu ya Simba ilimuuza mshambuliaji wake huyo tegemeo katika kikosi chake cha kwanza kwa miamba hiyo ya Tunisia pasipo kulipwa hata senti tano ubaoni.


Mbali na kutolipwa fedha yoyote ya uhamisho klabu ya Simba ilishindwa kupata mbadala wa Okwi na ikajikuta inapoteza mwelekeo, Etoile Du Sahel nayo ilishindwa kumtumia nyota huyo katika kikosi chake cha kwanza na kupelekea kumtelekeza.

Pia walishindwa kumlipa fedha zake za usajili ambazo ni jumla ya shilingi Mil 42, huku timu yake ya zamani Simba ikiachwa solemba na Mil 480 aidha Etoile Du Sahel ilishindwa kumlipa mshahara wake wa miezi mitatu.

Kwa mujibu wa taratibu za Fifa, klabu ya kulipwa ikishindwa kumlipa mchezaji wake mshahara wa miezi mitatu ni sawa na kuvunja mkataba, wakati klabu ya Simba ikipeleka mashitaka yake Fifa kutaka ilipwe fedha zake za usajili na klabu ya Etoile Du Sahel ya Tunisia.

Emmanuel Okwi naye aliishitaki Etoile Du Sahel akitaka kulipwa mshahara wake wa miezi mitatu huku akiendelea kusota, Etoile Du Sahel nayo ilifungua kesi Fifa ikimshitaki Okwi kwa utoro, Etoile imewasirisha kesi hiyo ikimtuhumu Okwi kwa kushindwa kujiunga na timu yao tangia alipoomba ruhusa ya kurejea kwao Uganda iliyokuwa na mchezo wa mchujo wa kombe la dunia dhidi ya Libya.

Hivyo kumefanya kuwepo kwa kesi tatu ndani ya shirikisho la kandanda duniani Fifa, wakati Fifa ikijiandaa kusikiliza kesi hizo, shirikisho la kandanda nchini Uganda FUFA nalo liliwasirisha barua maalum Fifa likiwaomba iwape Okwi kwa ruhusa maalum ili akacheze ligi ya kwao Uganda.

Lengo la FUFA lilitaka Okwi anusuru kiwango chake na apate fulsa ya kuitumikia Uganda katika michuano ya mataifa Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani maarufu CHAN, Fifa iliwapa kibali maalum FUFA ili kucheza soka Uganda.

SC Villa ilifanikiwa kumchukua Okwi kwa mkataba wa miezi sita, Fifa ilitoa masharti hayo kutokana na kuwepo kwa mgogoro baina ya Okwi na klabu yake ya Etoile Du Sahel ambapo pia kuna kesi tatu zinazomuhusu.

Wakati Okwi akitua katika klabu yake ya zamani ambayo ilimkuza na hatimaye kumuuza kwa Wekundu wa Msimbazi Simba SC, Villa ilitangaza kumuuza nyota huyo kwa mabingwa wa soka nchini Yanga.

Usajili huo wa Okwi uliibua mshangao kwa mashabiki wa soka nchini na kubwa zaidi Okwi kutua Yanga, wengi hawakuamini kwani klabu ya Simba haijalipwa fedha zake na Etoile Du Sahel ya Tunisia ambayo iliingia mkataba wa miaka miwili, usajili wa Okwi kutoka SC Villa ya Uganda kwenda Yanga ndio uliowashangaza wengi.

Lakini kama nilivyoanza mwanzo wa makala hii kuwa ukiyastaajabu ya Mussa utayaona ya Firauni, wengi wanaushangaa usajili wa Okwi kutoka SC Villa ya Uganda kwenda Yanga ya Tanzania wakati Simba ndio iliyomuuza kwa Watunisia.

Hapo sasa unapaswa kushangaa ya Firauni badala ya Mussa, klabu ya Simba moja kati ya timu maarufu katika ukanda huu wa CECAFA ilitangaza kumuuza mshambuliaji wake hatari na mwiba kwa wapinzani wake Emmanuel Okwi kwa Etoile Du Sahel ya Tunisia.

Kikubwa zaidi na cha kushangaza na kuwazodoa viongozi wa Simba walikubali vipi kumuuza Okwi ambaye alikuwa kipenzi cha Wansimbazi? kibaya zaidi Okwi ameuzwa bure huku fedha zikiishia hewani tu, mpaka sasa ni mwaka mmoja na nusu Simba haijalipwa chake, Simba inaidai Etoile Du Sahel dola za Kimarekani 300, 000 sawa na Mil 480 za Kitanzania.

Shutuma nyingi nazielekeza kwa mwenyekiti wa klabu hiyo Alhaj Ismail Aden Rage ambaye alijinasibu kwenye vyombo vya habari kuwa amemuuza Emmanuel Okwi kwa waarabu na Simba itaogelea noti huku akiikejeli Yanga ambayo nayo ilionyesha nia ya kumsajili.

Sakata la usajili huo usio na fedha ulizua sintofahamu nyingi kwa mashabiki wa soka nchini, kitendo cha Yanga kumsajili Okwi tena akitokea SC Villa ya Uganda badala ya Etoile Du Sahel ya Tunisia ambayo ndiyo iliyokuwa ikimmiliki kihalali.

Kitendo hicho kiliwaudhi Wanasimba na kufikia hatua ya kumnyooshea vidole mwenyekiti wao Ismail Rage, shirikisho la kandanda nchini TFF lilisimamisha usajili wa Okwi kwa klabu ya Yanga ili kutapa ipatiwe ufafanuzi na shirikisho la kandanda duniani Fifa hasa kuhoji uhalali wake kutoka Villa hadi kutua Yanga.

Hatimaye Fifa ilikata mzizi wa fitina na kutoa ufafanuzi wake ambapo ulimruhusu Okwi kukipiga Yanga, Yanga sasa wameruhusiwa kumtumia Okwi katika michuano ya kimataifa pamoja na ligi kuu bara, ruhusa hiyo ya Fifa inayomfanya Okwi kuichezea Yanga imeleta mshangao mkubwa.

Simba wameshangazwa na maamuzi ya Fifa, pia ikitakiwa kuvuta subira juu ya madai yake kwa Etoile Du Sahel ya Tunisia, rai yangu kwa Wanasimba nawaomba kutulia katika kipindi hiki kigumu wakati viongozi wakiendelea kufuatilia deni.

Uongozi wa Simba uliochini yake Rage naweza kuushangaa kama Firauni, Rage amefanya biashara zenye mshangao, amemuuza mshambuliaji kipenzi cha Wana Msimbazi bureee. pia amemuuza beki mahiri na tegemeo wa pembeni Shoimari Kapombe kwa klabu ya AS Cannes ya Ufaransa.

Mbaya zaidi staili iliyotumika kumuuza Okwi ndiyo iliyotumika kumuuza Kapombe, Kapombe ameuzwa bure, tayari Yanga wameanza chokochoko zao na wanamuhitaji kwa udi na uvumba ili kuimarisha kikosi chao.

Bila shaka usajili wa Okwi na Kapombe umetupa maarifa mapya, sidhani kama viongozi wajao wa Simba wanaweza kuthubutu kufanya biashara kama hiyo, mpaka sasa jitihada za kuunusuru usajili huo wa Okwi na Kapombe umeshashindikana kwa vile uhamisho wao umebarikiwa na Fifa hivyo Simba itegemee maumivu.