Licha ya Yanga kutolewa kwa mikwaju ya penalti 4-3 baada ya dakika 90 kumalizika timu hiyo ya Tanzania ikiwa imefungwa bao 1-0, hivyo kufanya matokeo ya jumla kuwa 1-1 kutokana na mchezo wa awali kikosi hicho cha Mholanzi Has van der Pluijm kuibuka na ushindi kama huo Uwanja wa Taifa, soka lililoonyeshwa na wachezaji hao liliwakosha Wamisri.
Katika mchezo huo uliofanyika mjini Alexandria, huku Al Ahly ikimiliki mpira kwa asilimia 65 dhidi ya 35 za Yanga, Dida alikuwa nguzo imara kwa kuokoa michomo mingi iliyoelekezwa langoni mwao huku Okwi akiisumbua safu ya ulinzi ya wapinzani wao.
Mbali na kuokoa michomo hiyo, Dida pia alikuwa kikwazo kwa Al Ahly wakati wa matuta baada ya kupangua penalti mbili, lakini Said Bahanuzi alishindwa kuhitimisha sherehe kwa Yanga kwa kufunga penalti ya mwisho.
Wakati Al Ahly ikiwa imepata penalti tatu baada ya kumaliza kupiga tano huku Yanga nayo ikiwa imeshatupia tatu lakini ikiwa na moja ya mwisho mkononi, Bahanuzi penalti yake ilikosa macho baada ya kupiga nje, hivyo kuingia piga nikupige ambapo Mbuyu Twite alikosa.
Kiwango hicho cha Dida kilimfanya mtangazaji wa mechi hiyo kila mara kumtaja huku akiomba Mungu kwa Lugha ya Kiarabu.
MECHI ILIVYOKUWA
Timu ya Yanga iliingia uwanjani ikiwa makini na kufanya mashambulizi kadhaa kwenye lango la Al Ahly lakini Mrundi, Didier Kavumbagu, alishindwa kutumia nafasi hiyo na mpira kuokolewa na walinzi kabla ya kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.
Al Ahly walifanya mashambulizi langoni mwa Yanga lakini safu ya ulinzi iliyo chini ya Kelvin Yondani, Nadir Haroub 'Cannavaro na Twite walikuwa makini kuokoa mashuti yaliyokuwa yanaelekea kwa Dida ambaye alikuwa akifanya kazi ya ziada kuokoa hatari.
Kutokana na uimara wa safu za ulinzi katika timu zote mbili, dakika 45 za kipindi cha kwanza zilimalizika kila upande ukiwa haujagusa nyavu za upande wa pili.
Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kufanya mashambulizi na kusaka mabao ya mapema, lakini bado ngome zote zilikuwa makini na kufanya milango kuwa migumu huku mwamuzi wa mchezo huo, Badara Diatta kutoka nchini Senegal akiwaonyesha kadi za njano wachezaji kadhaa wa Yanga.
Dakika ya 71 ya mchezo mlinzi wa kushoto wa Al Ahly, Sayed Moawad, aliipatia timu yake bao kufuatia mpira alioupiga kumzidi uwezo Dida na kujaa wavuni.
Mpaka dakika 90 za mchezo zinamalizika, Al Ahly 1 Yanga 0 na kufanya matokeo ya jumla kuwa 1-1 na hivyo timu hizo kuingia hatua ya matuta.
Wachezaji wa Yanga waliopata penalti hizo ni Nadir Haroub 'Cannavaro', Didier Kavumbagu na Okwi wakati Oscar Joshua, Bahanuzi, na Twite walikosa.
Penalti za Al Ahly zilifungwa na Abdalllah Said, Gedo, Trezeguet na Mohamed Nagieb huku Dida akipangua penalti mbili za Moawad na Hossan Ashour.
Yanga iliwachezesha: Dida, Twite, Oscar, Cannavaro, Yondani, Frank Domayo, Simon Msuva, Mrisho Ngasa/Athumani Idd 'Chuji', Kavumbagu, Okwi na Hamis Kiiza/ Bahanuzi.
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga, aliyefuatana na timu hiyo Misri, alisema juzi kabla ya mechi hiyo kwamba kikosi chao kitarejea nchini leo Jumanne kwa ndege ya Shirika la Ndege la Misri.