come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

MAKALA: HANS VAN DER PLUIJM NDIO WAKUPEWA PONGEZI,AMEIFIKISHA YANGA HAPA ILIPO

Na Fikiri Salum

YANGA imeweza kucheza kandanda la kuvutia na kushangaza wengi barani Afrika, kiwango ilichoonyesha mbele ya mabingwa wa kihistoria duniani Al Ahly ya Misri kimewashitua wadau wa soka.

Si maneno yangu isipokuwa takwimu za mchezo wa soka ndizo zinazosema, na inasemekana ndio mwisho tena kwa waarabu kupenda kuzipangia timu zao kucheza na timu za Tanzania pindi zinaposhiriki michuano ya Afrika.

Yanga ilicheza soka zuri lililoweza kuwachanganya waarabu na kujikuta wakipiga magoti na kuomba mungu ili waweze kupenya kwenye tundu la sindano.

Kama si penalti ya bahati mbaya ya Said Bahanuzi kupaa juu ya lango basi tungezungumza lugha nyingine, Katika mchezo huo wa marudiano uliochezwa Jumapili iliyopita, mabingwa watetezi wa ligi ya mabingwa Afrika Al Ahly ya Misri walipata ushindi wa bao 1-0.


Ushindi huo ulifanya matokeo yasomeke kuwa 1-1 baada ya Yanga kutangulia kushinda bao 1-0 katika mchezo wa mkondo wa kwanza uliofanyika jijini Dar es Salaam wiki moja iliyopita.

Shukrani za pekee zimuendee beki na nahodha wa timu hiyo Nadir Haroub Ally 'Cannavaro' ambaye alifunga goli pekee kwa upande wa Yanga na kuondoa mkosi wa kutowafunga waarabu.

Licha ya Yanga kutolewa katika michuano hiyo ya Afrika mwaka huu lakini inahitaji kupongezwa kutokana na kuchezxa kandanda la kuvutia na kuonyesha ushindani wa hali ya juu.

Ushindani huo umewashitua waarabu kiasi kwamba kutoamini macho yao, Jumapili iliyopita katika ardhi yao huko Alexandria Misri, kikosi cha Yanga kiliweza kutawala mchezo ingawa ilipoteza kwenye mikwaju ya penalti.

Tuseme Yanga haikuwa na bahati katika mikwaju ya penalti lakini ilicheza soka la kuvutia, makali ya washambuliaji wake Hamis Friday Kiiza, Simon Msuva, Said Bahanuzi, Emmanuel Okwi na Mrisho Ngasa uliweza kuwapa tumbo joto waarabu.

Safu ya ulinzi ya Yanga iliongozwa vema na nahodha wake Nadir Haroub 'Cannavaro' akisaidiana na Kelvin Yondani 'Vidic', mabeki hao wa kati walisaidiana vema na walinzi wa pembeni ambao ni Mbuyu Twite (kulia) na Oscar Joshua (kushoto).

Kiungo wa katikati anayesifika kwa siku za hivi karibuni Frank Domayo ameonekana kuwadhibiti Al Ahly kuanzia mechi ya kwanza hadi marudiano.

Siyo siri Yanga imeimarika, siyo ile iliyocheza na Simba na kufungwa magoli 3-1 kwenye mechi ya Hisani iliyojulikana kamaNani mtani Jembe iliyochezwa uwanja wa Taifa Desemba 21 mwaka jana.

Katika mchezo ule Yanga ilipokea kichapop kitakatifu cha mabao 3-1 na kupelekea kufukuza benchi zima la ufundi, Yanga ilimfuta kazi kocha wake mkuu Mholanzi Ernie Brandts pamoja na wasaidizi wakeFred Minziro na Razack Ssiwa.

Pia ilimtimua daktari wake Nassoro Matuzya, nafasi zao zilizibwa na Hans Van Der Pluijm raia wa Uholanzi ambaye amekuwa kocha mkuu na msaidizi wake ni Charles Boniface Mkwasa.

Aidha Juma Pondamali aliteuliwa kuwa kocha wa makipa na Juma Sufiani akawa daktari wa timu, uteuzi huo ulifuatiwa na ziara ya mafunzo nchini Uturuki ambapo kikosi kizima cha timu hiyo kiliondoka.

Wakati Yanga ikiondoka kuelekea Uturuki, huku nyuma wadau wa soka walikibeza kitendo hicho cha kuondoka huku wengine wakiizodoa na kudai imekimbia kivuli chake, Yanga ilijitoa kwenye michuano ya Mapinduzi Cup ambapo mtani wake Simba ilishiriki na kushika nafasi ya pili.

Ziara ya Uturuki imeweza kuisaidia Yanga hatimaye kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa pamoja na ligi kuu bara, Yanga ilianza michuano ya kimataifa kwa kuilaza Komorozine ya Comoro mabao 7-0 katika mchezo wa kwanza uliofanyika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Timu hizo zilirudiana wiki moja ijayo ambapo Yanga ilisafiri hadi mjini Moroni mji mkuu wa Comoro, katika mchezo wa marudiano Yanga iliibuka mshindi kwa mabao 5-2 na kusonga mbele kwa jumla ya mabao 12-2.Iliporejea nchini Yanga ilicheza mchezo wa ligi kuu bara ambapo iliishushia kipigo kitakatifu Ruvu Shooting ya Pwani mabao 7-0 na kuweka rekodi mpya katika uwanja wa Taifa na kuwa timu kwanza kushinda idadi ya mabao hayo.

Yanga imeonekana kubadilika zaidi sehemu mbalimbali ndani ya uwanja, kocha mpya Hans Van Der Pluijm anaonekana yuko makini zaidi kuliko makocha wote waliopata kuinoa timu hiyo, Pluijm ni fundi wa kweli wa soka ambapo Wanayanga kama watamtumia ipasavyo Yanga inaweza kufika mbali.

Kocha huyo ameweza kuwabadili wachezaji mmoja mmoja na kuimarisha viwango vyao ambapo katika siku za hivi karibuni walionekana kuchuja, Nadir Haroub 'Cannavaro' kwa sasa yuko katika kiwango cha juu mara mbili ya kile alichowahi kuwa nacho.

Ni matunda ya Pluijm hayo, Emmanuel Okwi huyu wa Yanga ni mara mbili ya yule wa Simba ambaye akiiongoza kuiua Yanga mabao 5-0 katika uwanja wa Taifa mchezo wa ligi kuu Tanzania bara, kwanza Okwi yule aliikuta Yanga iko kwenye migogoro ya kiutawala ambapo aliyekuwa mwenyekti wa Yanga kipindi hicho Lyoid Nchunga alitakiwa kujiuzuru.

Pljuim amemfanya Okwi kuongezeka makali sambamba na wachezaji wengine akiwemo Oscar Joshua ambaye kiwango chake kilipotea enzi za Brandts na Minziro.

Sina maswali kwa Deo Munishi 'Dida' ambaye mechi alizocheza ni kielelezo chake cha kupanda kiwango, Pluijm ameisaidia Yanga kushinda magoli mengi na kuandika rekodi ya aina yake, pia Yanga imeanza kuzitisha klabu nyingine za ligi kuu.