come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

TUKO TAYARI KUJIUNGA AL AHLY- CANNAVARO, DIDA

Nyota wawili wa Yanga, beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na kipa Deogratius Munishi ‘Dida’ wamesema wapo tayari kujiunga na klabu ya Al Ahly ya Misri ambayo imeonyesha nia ya kutaka kuwasajili.

Cannavaro alisema taarifa za kutakiwa na Ahly alizipokea kwa mikono miwili, na amewaomba viongozi wa klabu yao kutowawekea ugumu katika kukamilisha uhamisho huo ili waende kupandisha viwango vyao katika klabu hiyo ambayo ni mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Hakuna atakayeweza kukataa kujiunga na Al Ahly, hii timu ni kubwa ukisikia wanakuhitaji ni wazi utafurahia taarifa hiyo, nipo tayari kuondoka Yanga hata sasa, naipenda Yanga, ombi langu kwa viongozi wa klabu wasiweke ugumu katika mazungumzo yao na uongozi wa Al Ahly,” alisema Cannavaro ambaye ni nahodha wa Yanga.


Naye Dida kwa upande wake alisema taarifa za kutakiwa na Ahly amezipokea kwa faraja kubwa.

“Nimezipata taarifa hizo, zimenipa faraja, kama unavyojua hiyo ni timu kubwa hapa Afrika, sina pingamizi kama Al Ahly watakubaliana na waajiri wangu Yanga, hakuna shida. Naomba viongozi wawe waelewa katika hilo,” alisema Dida.

Uongozi wa Yanga umekiri Al Ahly kuonyesha nia ya kutaka kuwasajili Dida na Cannavaro, lakini uligoma kutaja dau linalohitajika kuwang’oa wachezaji hao.

Kaimu Mwenyekiti wa Mashindano wa Yanga, Mussa Katabaro alisema tayari Al Ahly imefanya mazungumzo ya awali na uongozi wa Yanga ikionyesha nia yao ya kuwataka nyota hao, lakini Yanga imewataka kuwasilisha barua rasmi ya maombi hayo. Katabaro alikuwa Misri sambamba na Makamu Mwenyekiti wa timu hiyo, Clement Sanga ambaye naye akiri kuwapo kwa mpango huo.

Wakati huohuo, kikosi cha Yanga kimetua jana saa 12:00 alfajiri jijini Dar es Salaam kikitokea nchini Misri na kocha wa Yanga, Hans Van Pluijm aliamua kuvunja mapumziko kwa wachezaji wake na kuwataka jana jioni waanze mazoezi kwa ajili ya kujiandaa na mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Mtibwa Sugar.