come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

RAGE AIKASHIFU SIMBA, ATAMBA KUTOGOMBEA UENYEKITI, ADAI YEYE SI MASIKINI

Wakati wanachama wa Simba wakipitisha mapendekezo ya marekebisho ya katiba yao, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ismail Aden Rage ametangaza kutogombea tena nafasi hiyo jana asubuhi kwenye ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa Polisi, Oysterbay.

Akizungumza kwenye mkutano huo wa marekebisho ya Katiba ya Simba, Rage alisema: “Simba oyee...Wanasimba msifanye makosa Mei 4 hakikisheni mnachagua kiongozi ambaye atakaa madarakani miaka minne, msifanye makosa baada ya mwaka mmoja mkataka aondoke, Katiba ya Simba inakataza mapinduzi.

“Mimi sitagombea, mimi siyo maskini, sina njaa, hata mkizomea nasemaje mimi sina njaa, na wanachama wengi mliopo hapa ni mambumbumbu.”

Kauli hiyo iliamsha hasira kwa baadhi ya wanachama ambao walitaka kumvamia na kumtwanga makonde, lakini Polisi waliingilia kati na kusababisha wanachama kupambana na wale wanaomuunga mkono Rage, tafrani hiyo ilidumu kwa zaidi ya nusu saa hadi pale Rage alipoomba radhi kwa kutangaza kuifuta kauli yake hali ikatulia na mkutano ukaanza.


Hata hivyo mkutano huo ulifanyika huku akidi ya wanachama ikiwa haijatimia kwani ili akidi itimie ilitakiwa kuwe na wanachama 250 na kuendelea, lakini wanachama waliofika jana ni 166 ambao hawafikii hata nusu ya akidi ya wanachama ambayo inatambulika kwa mujibu wa Katiba ya Simba.

Katika mkutano huo wanachama walipinga kuburuzwa kwa kuwepo kipengele cha ibara ya 11 (a) ambacho kinakataza mwanachama kuzungumza na vyombo vya habari isipokuwa vikao halali, na mwanachama atakayefanya hivyo tawi limuwajibishe ndani ya siku 14 tangu kutokea kwa kitendo hicho, wanachama hao waligoma na kutaka kifungu hicho kiondolewe kwani kinawaminya uhuru na haki ya kuzungumza.

Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Geofrey Nyange naye alijikuta akizodolewa na Rage pale aliponyoosha kidole na kusema: “Taarifa mwenyekiti...taarifa, huku akisimama na kujibiwa na Rage ‘Siyo lazima usimame, kaa chini, nimesema siyo lazima, mwingine’ alisema Rage na kuteua mwanachama mwingine kuchangia hoja yake kabla ya kumpa nafasi Kaburu.

Akichangia kuhusu kipengele hicho Kaburu alisema: “Hakuna eneo ambalo TFF ilisema kuhusu kifungu hiki, haya ni mawazo yetu ni kweli baadhi ya wanachama wanatukana viongozi ndio maana kikawekwa ili kuminya wanachama wakorofi, kwa vile tupo hapa kwa ajili ya kuunda Kamati ya Maadili wakorofi wote watapelekwa kamati ya maadili ndio watawajibishwa huko siyo kuingiza kwenye katiba,” alisema Kaburu na kushangiliwa na wanachama wengi.

Kipengele kingine ambacho kinasubiri huruma ya TFF ambacho Simba wamekipitisha kwa kishindo ni kile cha ibara ya 26 kinachozungumzia sifa za wagombea, fasili ya tano ya katiba ya Simba ya zamani inasomeka: ‘Asiwe aliyewahi kutiwa hatiani kwa kosa la jinai kwa kuhukumiwa kifungo’.

Wanachama hao wametaka kifungo hicho kisomeke ‘Asiwe ametiwa hatiani kwa kifungo cha zaidi ya miezi sita bila mbadala wa adhabu na endapo ametiwa hatiani kwa kifungo cha zaidi ya miezi sita, awe amemaliza muda wa miaka mitano tangu kuisha kwa kifungo husika bila kutiwa hatiani kwa kosa lingine lolote la jinai.

Kipengele hicho (b) kimeongezwa maneno yanayosomeka: ‘Mgombea ni lazima awe ametimiza angalau mwaka mmoja wa uanachama na si miaka mitano kama ilivyo sasa.