come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

YANGA WAIVUTIA KASI AZAM JUMATANO, DIDA, NGASA WAREJEA KUISHIKA.

YANGA SC imeingia kambini katika hoteli ya Kiromo, Bagamoyo mkoani Pwani jana moja kwa moja ikitokea Morogoro ambako juzi ilitoa sare ya bila kufungana na Mtibwa Sugar Uwanja wa Jamhuri, katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

Yanga SC imeingia kambini Bagamoyo kujiandaa na mchezo wake ujao wa ligi hiyo, dhidi ya Azam FC utakaofanyika Jumatano Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kipa Deo Munishi ‘Dida’ aliyekosekana katika mchezo wa Jumamosi baada ya kuumia mazoezini anaweza kuanza mazoezi kesho, wakati Mrisho Ngassa aliyeumia katika mchezo dhidi ya Al Ahly mjini Alexandria, Misri alikwenda kupumzika Mwanza na anatarajiwa kurejea Dar es Salaam leo, ingawa uhakika wa kucheza Jumatano haupo.

Ngassa alitoka nje kipindi cha pili wiki iliyopita Uwanja wa Border Guard, Yanga SC ikitolewa katika Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa penalti 4-3 kufuatia sare ya jumla ya 1-1 baada ya kila timu kushinda 1-0 nyumbani kwake na alipotua Dar es Salaam akaenda nyumbani Mwanza.


Pamoja na kulazimishwa sare na Mtibwa juzi, Yanga SC ilicheza nyuma ya bahati Uwanja wa Jamhuri, kwani ilitawala mchezo na kukosa mabao zaidi ya matatu ya wazi.

Kipa aliyesajiliwa maalum kwa mashindano ya kimataifa, Juma Kaseja baada ya kukosa mechi tatu mfululizo za Ligi ya Mabingwa, moja dhidi ya Komorozine mjini Moroni na mbili dhidi ya Al Ahly Dar na Alexandria alionyesha yuko vizuri kwa kudaka vyema- maana yake hata kama Dida hatakuwa tayari kwa mchezo wa Jumatano, bado lango la Wana Jangwani litakuwa kwenye mikono salama.

Yanga SC inayofundishwa na kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm ilipata msukosuko kidogo wakati inatokea Morogoro asubuhi ya jana, baada ya basi lake kuacha njia kidogo wakati linajaribu kukwepa basi la abiria lililopoteza mwelekeo eneo la Mikese.

Hata hivyo, halikupinduka- bali tairi za upande mmoja ziliingia kwenye bonde dogo pembezoni mwa barabara na saa moja ilitosha kulirejesha barabarani kuendelea na safari hadi Bagamoyo.

Azam FC baada ya juzi kuichapa mabao 4-0 Coastal Union ya Tanga Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam jana nayo imeingia kambini katika hosteli zake za Chamazi.

Kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog aliamua kwa makusudi kumpumzisha Mganda Brian Umony katika mchezo wa juzi kwa ajili ya mchezo wa Jumatano.

Mchezaji mwenye bahati ya kuwafunga Yanga SC, John Bocco ‘Adebayor’ ameonyesha sasa yuko fiti kabisa baada ya kucheza vyema juzi na kufunga bao moja Chamazi.
 
Pengo lililoonekana kutaka kuisumbua Azam la beki ya kushoto kufuatia wachezaji wote wa nafasi hiyo Samih Hajji Nuhu na Waziri Salum kuwa majeruhi kwa muda mrefu, sasa linaonekana kuzibwa vyema na beki aliyepandishwa kutoka kikosi cha pili, Gadiel Michael.

Yanga na Azam kwa sasa haswa ndizo zinazofukuzana kwa kasi kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

Azam wako mbele ya Yanga SC kwenye mbio hizo kwa pointi 43 walizovuna kwenye mechi 19, wakati wapinzani wao hao wana pointi 39 baada ya mechi 18.

Azam FC iliifunga Yanga SC mabao 3-2 katika mchezo uliopita wa Ligi Kuu Uwanja wa Taifa, ikitoka kufungwa 1-0 na mabingwa hao wa Bara katika mchezo wa Ngao ya Jamii hivyo mchezo wa Jumatano utakuwa ni wa kusaka mbabe wa jumla wa msimu baina yao.

Lakini pia mchezo huo unaweza kutoa taswira nyingine ya mbio za ubingwa, kwani atakayeshinda ndiye atapanda kileleni- kwa Azam ni muhimu kushinda kwa sababu wamecheza mechi moja zaidi ya Yanga SC.