MSHAMBULIAJI wa kutumainiwa wa mabingwa watetezi wa ligi kuu Tanzania bara Mganda Emmanuel Okwi amezipinga kauli zinazotolewa na baadhi ya vyombo vya habari nchini kuwa ameikimbia Yanga kama alivyofanya kwa klabu ya Etoile Du Sahel ya Tunisia.
Okwi amefafanua kuwa maumivu aliyoyapata wakati timu yake ilipocheza na Prisons ndiyo yaliyopelekea kushindwa kuingia kambini kuungana na wenzake katika kuhakikisha wanatetea ubingwa wao, Okwi amedai tangia alipoumia katika mchezo huo hali yake ilikuwa si nzuri licha ya kucheza mechi yao dhidi ya Mgambo JKT.
Hata hivyo Okwi amedai yeye bado ni mchezaji wa Yanga na ataendelea kuitumikia timu yake hiyo kwakuwa bado ana mkataba nayo tena mrefu wa miaka miwili na nusu, kuikacha Yanga ni kosa kubwa hivyo anawataka washabiki na wapenzi wa Yanga kutoamini kauli hizo.
'Mimi ni Yanga siwezi kukimbia nashangaa sana kauli hizi zinatolewa wakati wanajua fika kuwa niliumia katika mchezo ule dhidi ya Prisons na nilishindwa kuendelea, tunajiandaa na Simba maneno mengi yanavumishwa juu yetu ili kutuharibu kisaikolojia', alisema Okwi.