Ushindi uliifanya Yanga kufikisha pointi 49, nne nyuma ya Azam huku zikiwa zimebaki mechi tatu ligi kumalizika. Mbeya City ilibaki katika nafasi ya tatu kwa kuwa na pointi 46 huku ikiwa imecheza mechi moja zaidi ya vinara hao wawili, huku Simba itulia katika nafasi ya nne kwa pointi zao 37, baada ya sare yao ya juzi ya 1-1 dhidi ya Kagera Sugar.
Mgambo JKT iliendelea na kasi yake ya kujinasua kutoka katika ukanda wa kushuka daraja wakati ilipowachapa wapinzani wao wa Tanga, Coastal Union kwa magoli 2-0 na kufikisha pointi 25 zilizowapandisha hadi katika nafasi ya 10 katika ligi hiyo ya timu 14 inayoteremsha daraja timu tatu.
Mgambo kwenye uwanja wa Mkwakwani katika mzunguko wa pili umezichapa timu za Simba na Yanga pia. Katika mechi nyingine ya jana, JKT Oljoro ilishinda 2-1 dhidi ya Tanzania Prisons.
Ngasa alianza vitu vyake jana mapema katika dakika ya tisa wakati alipoifungia Yanga goli la kwanza akimalizia pasi murua ya mguu wa kushoto iliyopenyezwa na mshambuliaji Mrundi Didier Kavumbagu ndani ya boksi.
Katika robo saa ya mechi Ngasa alirudi tena nyavuni akimalizia kwa shuti hafifu mpira uliotemwa na kipa Shabani Dihile kufuatia shuti kali la Kavumbagu aliyepenyezewa pasi na winga wa kulia Simon Msuva. Kazi nzuri ilifanywa na Kiiza kabla ya pasi hiyo.
Dakika nne kabla ya mapumziko, Kavumbagu alipatia Yanga goli la tatu akiitendea haki pasi safi ya Ngasa ndani ya boksi na kuzifanya timu hizo zipumzike wenyeji wakiwa mbele kwa magoli 3-0.
Ngasa alikamilisha 'hat-trick' yake ya kwanza msimu huu katika dakika ya tatu kipindi cha pili baada ya kupiga shuti kali la mguu wa kulia akiwa nje ya boksi lililomshinda kipa Dihile.
Mtokea benchi Hussein Javu alifungia Yanga bao kali la tano akikimbia kwa kasi kutoka katikati ya uwanja kabla ya kupiga shuti kali lililotinga nyavuni katika dakika ya 51.
Ilikuwa ni 'hat-trick' ya tatu kwa Ngasa msimu huu baada ya kufunga magoli matatu-matatu mara mbili katika mechi mfululizo za hatua ya kwanza ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Komorozine ya Comoro.
Pia ilikuwa ni 'hat-trick' ya tano katika Ligi ya Kuu ya Vodacom msimu huu pamoja na 'hat-trick' mbili za Amisi Tambwe wa Simba, Abdallah Juma wa Mtibwa na Mwegane Yeya wa Mbeya City.
JKT walijitutumua na kupata bao la kufutia machozi lililofungwa kwa kichwa na Nashon Naftali akiunganisha krosi kutoka kwa Damas Makwaya dakika saba kabla ya mechi kumalizika.
Katika mechi hiyo, Yanga ilimkosa beki wake wa kikosi cha kwanza Kelvin Yondani kutokana na kuwa na kadi tatu za njano.
Vikosi vilikuwa; Yanga: Deogratius Munishi 'Dida', Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub 'Cannavaro', Mbuyu Twite, Frank Domayo, Simon Msuva, Hassan Dilunga/ Hamis Thabit (dk.77), Didier Kavumbagu/ Jerson Tegete (dk.67), Mrisho Ngasa na Hamis Kiiza/ Hussein Javu (dk 45)
JKT Ruvu: Shabani Dihile, Damas Makwaya, Edward Charles, Omar Mtaki, Jamal Machelanga, Nashon Naftal, Sino Agustino, Emmanuel Swita, Idd Mbaga, Hussein Bunu/ Amos Mgina (dk.50) na Karage Mgunda/ Samwe Kamutu (dk.60)
NGORONGORO SARE
Kwenye Uwanja wa Kenyatta (Machakos) Ngorongoro Heroes imetoka suluhu na Kenya U2O. Timu hizo zitarudiana Uwanja wa Taifa Aprili 27 mwaka huu. Mshindi atacheza dhidi ya Afrika Kusini katika hatua ya pili kuwania kufuzu Fainali za Africa kwa U20 Senegal kuanzia Julai mwaka huu.