Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Emil Malinzi amesema leo kwamba, wametuma barua kwa klabu yao, TP Mazembe kuwaomba kwa ajili ya mchezo huo, lakini hawajajibiwa.
“Tulituma barua, lakini tunasikitika hadi sasa hatujajibiwa na hatujui hatima ya wachezaji hao, ila kwa vyovyote tunajipanga vizuri kwa ajili ya mchezo huo hata bila ya wao,”alisema Malinzi.
Wachezaji hao wa Tout Puissant Mazembe ya DRC walikuja katika mchezo wa kwanza wa mchujo kuwania kupangwa kwenye makundi ya kugombea tiketi ya AFCON 2015 nchini Morocco Taifa Stars ikishinda 1-0 wiki iliyopita.
Juzi walikuwa wana mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika nyumbani Lubumbashi dhidi ya AS Vita ya Kinshasa na Samatta akafunga bao pekee la ushindi.
Mazembe watakuwa na mchezo mwingine Juni 7 dhidi ya Zamalek ya Misri wakicheza nyumbani tena, Lubumbashi na wikiendi hii hawatakuwa na mchezo- maana yake hawataathirika kuwaruhusu nyota hao kuja kuitumikia nchi yao.
Lakini baada ya kufungwa mechi moja na kushinda moja katika Kundi lake A Ligi ya Mabingwa Afrika, Mazembe inaweza kuhitaji kuwa na maandalizi mazuri ya pamoja na wachezaji wake wote kwa ajili ya mechi na Zamalek.
Kama itakuwa hivyo, basi Taifa Stars itawakosa wachezaji wake hao muhimu katika mchezo huo mgumu, ambao watakuwa na jukumu la kulinda ushindi mwembamba wa 1-0 ulitokana na bao la John Bocco wa Azam FC.