come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

WAMBURA ATANGAZA HALI YA HATARI SIMBA

Michael Wambura, mgombea wa urais katika uchaguzi wa Simba aliyeenguliwa na kamati ya uchaguzi ya klabu hiyo, amesema anakata rufaa leo katika Shirikisho la Soka nchini (TFF) kupinga maamuzi hayo.


Wambura ameondolewa kushiriki katika kinyang'anyiro hicho na Kamati ya Uchaguzi ya klabu hiyo kwa maelezo kuwa si mwanachama wa Simba kwa vile alisimamishwa rasmi na Kamati ya Utendaji ya Simba Mei 5, 2010 baada ya kufungua kesi ya suala la soka katika mahakama za kiraia na hajarejeshwa na mkutano mkuu kama Katiba ya Simba inavyosema.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye jengo la klabu hilo lililopo Kariakoo jijini Dar es Salaam jana, Wambura ambaye wafuasi wake jana walifunga mitaa huku wakizungumza na askari wa kutuliza ghasia (FFU), alisema hakubaliani na maamuzi hayo na leo saa tano asubuhi atatinga kwenye ofisi za TFF kuwasilisha rufaa yake dhidi ya Kamati ya Uchaguzi ya Simba inayoongozwa na Damas Ndumbaro.

"Mkutano wa Kamati ya Utendaji ya Simba uliofanyika 2010 kunisimamisha uachama ulikuwa batili kwa sababu haukuitishwa na mwenyekiti na baadhi ya wajumbe hawakuhudhuria lakini saini zao zilighushiwa," alisema.

"Hata walioniwekea pingamizi katika Kamati ya Uchaguzi ya Simba wengi wao wanatoka kwenye Tawi la Mpira Pesa ambalo limeshafutwa uachama wa Simba.

"Mimi ni mwanachama hai wa Simba kwa sababu Katiba yetu inasema mtu anapoteza uhai wa uanachama wake Simba endapo atafariki, kushindwa kulipa ada ya uanachama au kufukuzwa na mkutano mkuu wa wanachama. Mimi sijawahi kufukuzwa kwa sababu hakuna mkutano mkuu wa Simba uliokaa na kufikia maamuzi hayo.

"Sijawahi kupata barua hata ya kusimamishwa uachama na kwa muda wote nimeendelea kulipa ada ya uanachama. Nimeshiriki katika uteuzi wa wajumbe wa Kamati ya Uchaguzi ya Simba nikiwa kama mjumbe wa Kamati ya Utendaji. Kama mimi si mwanachama wa Simba maana yake hata uteuzi huo ni haramu. Kwa nini wamekubali uteuzi huo wakati mimi si mwanachama wa Simba?" Alihoji Wambura.

OFISI MSIMBAZI ZAFUNGWA

Katika hatua nyingine, baadhi ya wapenzi wa klabu hiyo waliodai kumuunga mkono Wambura walifunga geti la kuingilia kwenye ofisi za makao makuu ya klabu hiyo wakishinikiza mgombea huyo arejeshwe.

"Ili tufungue hapa inabidi kamati imruhusu Wambura kugombea na kiongozi pekee wa Simba anayeruhusiwa kuja kufungua hapa ni Rage (Aden, ambaye ni Rais wa klabu hiyo)," alisema mmoja wa wa mashabiki hao waliokuwa wamefurika kwenye ofisi hizo na mitaa ya Kariakoo.