Wakati mgombea wa nafasi ya Urais katika Uchaguzi Mkuu wa Klabu ya Simba, Michael Wambura, akiwa ameondolewa kwenye mchakato wa kuwania cheo hicho, ameibuka na kusema kwamba hana hofu yoyote na maamuzi yatakayotangazwa leo na Kamati ya Uchaguzi ya klabu hiyo ya Wekundu wa Msimbazi.
Wambura alikuwa ni mmoja wa wagombea waliowekewa pingamizi na wanachama wa Simba na juzi alihojiwa na kamati hiyo iliyoko chini ya Mwenyekiti wake, Damas Ndumbaro.
Akizungumza jana, Wambura, alisema baada ya kuwapo kwa 'fununu' kutoka kwa kamati hiyo za yeye kutemwa na kamati hiyo, hana wasiwasi wowote na kwamba anasubiri taarifa rasmi ili ajue anachukua maamuzi yapi.
Wambura alisema kuna watu hawataki yeye awanie uongozi ndani ya klabu hiyo na dalili hizo zilianza pale alipowekewa pingamizi na wanachama watano wa Simba.
Alisema ni mapema kwa jana kuzungumza chochote, mpaka pale atakapopata taarifa kutoka kwa kamati na anaamini wajumbe wa kamati hiyo watatenda haki.
"Kuna watu wanataka nisigombee, kuwekewa pingamizi na watu watano ni dalili tosha za kutaka kunikwamisha, ila kwa sasa siwezi kusema kitu, wacha tuvuke mto kwanza, huwezi kusema kitu kabla hujavuka mto wenyewe," alisema Wambura ambaye aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Tanzania (FAT sasa TFF).
Hata hivyo, mwishoni mwa wiki Wambura akihojiwa na Kituo cha Televisheni cha ITV alisema baadhi mambo yanayoendeshwa na kamati hiyo ya uchaguzi yanaenda kinyume cha taratibu za uchaguzi zilizowekwa.
Alitoa mfano kamati hiyo kukataa kuweka wazi pingamizi walizowekewa kwa sababu kwa kufanya hivyo inawanyima nafasi wale waliopingwa kuandaa utetezi.
Habari kutoka ndani ya kamati hiyo zinaeleza kwamba wagombea wa nafasi ya Makamu wa Rais, Geofrey Nyange 'Kaburu', Joseph Itang'are 'Kinesi' na Swedy Nkwabi ambao waliwekewa pingamizi wameweza kujitetea vyema na majina yao yataendelea kuwapo katika mchakato wa kuwania uongozi.
TAARIFA RASMI LEO
Kamati ya Uchaguzi leo inatarajia kutangaza maamuzi yake baada ya kuwahoji wagombea wote waliowekewa pingamizi na wanachama wa klabu hiyo.
Ndumbaro alisema jana kuwa leo wataeleza maamuzi yao kwa kuzingatia kanuni na Katiba ya Simba na si nje ya hapo.
"Kila tutakachokifanya kitakuwa ni kutokana na katiba na kanuni zinavyosema na si maamuzi ya mjumbe wa kamati hii," Ndumbaro alieleza.
Alisema baada ya kupitia mapingamizi, zoezi la usaili ndio linafuata na litafanyika keshokutwa Alhamisi kwenye Ukumbi wa Bwalo la Polisi Oysterbay jijini.
Uchaguzi Mkuu wa Simba unatarajiwa kufanyika Juni 29, mwaka huu baada ya viongozi waliopo madarakani kumaliza muda wao kwa mujibu wa katiba.